Huyu ndiye Tundu Lissu


Kutoka mafichoni ubalozini hadi Ubelgiji, Mwandishi Diramakini anakujuza...
Aliyekuwa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Tundu Lissu, amewasili nchini Ubelgiji leo Jumatano Novemba 11, 2020.

Aliondoka jijini Dar es Salaam jana Jumanne saa 11 jioni kwa ndege ya shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines). 

Katika Uchaguzi Mkuu huo wa Oktoba 28, 2020, mgombea huyo alishika nafasi ya pili, nyuma ya mgombea wa chama tawala Cha Cha Mapinduzi (CCM), Mhe.Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ambaye aliibuka mshindi kwa asilimia 84.4 huku Lissu akiambulia asilimia 13.

Aidha, yakiripoti kuwasili kwa Lissu nchini Ubelgiji, mashirika mbalimbali ya habari duniani yamekariri taarifa ya Shirika la habari la Ufaransa (AFP) likisema kwamba kiongozi huyo wa upinzani aliwasili Ubelgiji akitokea nyumbani kwa Balozi wa Ujerumani jijini Dar es Salaam.

Mashirika hayo yakionekana kufuatilia safari hiyo yalimkariri Lissu akisema kwamba alipanda ndege ya shirika la ndege la Ethiopia jijini Dar es Salaam, ambapo kabla ya kuwasili Ubelgiji ilitua katika miji ya Addis Ababa (Ethiopia) na Vienna (Austria).

Itakumbukwa kuwa, baada ya kutangazwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu, Lissu alikimbilia kwenye ubalozi wa nchi ya Ujerumani jijini Dar es Salaam na kwendelea kuishi hapo, akidai kuwa alikuwa amepokea vitisho kutoka 'kusikojulikana' dhidi ya maisha yake.

AFP ilimkariri mke wa Lissu, Alicia Magabe, akiiambia kuwa mumewe amekuwa akijificha kwenye ubalozi huo wa Ujerumani tangu Novemba 2, mwaka huu.

Kadhalika, katika mwendelezo wa taarifa hiyo ya AFP, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt.Donald Wright amesema, Lissu aliondoka jana nchini kwenda kwenye matibabu, ambapo pia shirika hilo limekariri chanzo kingine ambacho hakikutajwa ikikanushwa kuwa si kweli kwamba kiongozi huyo amekwenda Ughaibuni kwa ajili ya matibabu.

Lissu mwenyewe katika mahojiano na AFP kabla ya kuondoka jijini Dar es Salaam, alisema kuwa anaondoka kwa sababu za kiusalama na pia kwenda kutibiwa.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA), Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), alisindikizwa na maofisa wa Ubalozi wa nchi za Ujerumani na Marekani, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.

Kwa upande mwingine, akizungumza na mtandao wa habari wa 'MwanaHALISI Online' mapema kabla ya kupanda ndege, Lissu alisema ameamua kuondoka nchini ili kunusuru maisha yake na “kujipanga upya kisiasa.”

Itakumbukwa kuwa Lissu alirejea nchini Julai 27, 2020, kutokea nchini Ubelgiji, na kujitumbukiza moja kwa moja kwenye kinyang’anyiro cha Urais wa Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news