Comoro yaipongeza Tanzania kwa kufanya uchaguzi huru, amani na haki

Rais wa Visiwa vya Comoro, Azali Assouman ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanya uchaguzi huru, amani na haki.

Ameipongeza Tanzania leo Novemba 10,2020 jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa tayari kwa kuondoka nchini na kurejea Comoro baada ya kushuhudia uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli uliofanyika Novemba 5, mwaka huu jijini Dodoma.

Rais Assouman amesema, Tanzania ni nchi ya amani na utulivu wa kisiasa kwani wakati wote wa tukio la kuapishwa kwa Dkt.Magufuli aliona mambo ambayo yanapaswa kuigwa na mataifa mengine hususani kwenye nyakati za uchaguzi.

"Kwa kweli tangu nimefika hapa Tanzania nimeona mambo mazuri na ambayo tunapaswa kuyaiga sisi viongozi wa mataifa mengine,"amesema Rais Assouman.

Mbali na kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi, pia Rais Assouman aliahidi ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo diplomasia ya uchumi, biashara, uwekezaji na utalii.
Rais wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Azali Assouman akiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), baada ya kushuhudia  hafla ya uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli iliyofanyika Novemba 5, 2020, katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma na baadaye alitembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

“Najisikia niko nyumbani kwa sababu uhusiano wetu umeimarishwa zaidi, mahusiano yetu yamekuwa katika masuala ya kijamii, utamaduni, biashara na mambo mengine mengi,"amesema Rais Assouman.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Comoro,Sylvester Mabumba amesema kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Comoro katika kuhakikisha kuwa sera ya uchumi wa nchi zote mbili unakua zaidi. 

"Sisi tuatendelea kushirikiana vyema na Comoro kibiashara ili kukuza sera ya 2025 tunaifikia ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa uchumi wetu unafikia kiwango cha juu sana, ninaamini kuwa tunapokuwa na masoko ya uhakika Viswa vya Comoro uchumi wetu utakuwa zaidi,"alisema Balozi Mabumba.

Kwa upande wake Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania, Dkt. Ahmada El Badaoui Mohammed alisema kuwa, kuna fursa nyingi za kiuchumi ambazo Comoro na Tanzania zinaweza kushirikiana.

Rais Assouman aliwasili nchini Novemba 4, mwaka huu kwa ajili ya kuhudhuria hafla ya uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli uliofanyika Novemba 5 Jijini Dodoma ambapo baada ya shughuli hiyo alipata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na kujiona vivutio mbalimbali vya utalii nchini.

Serikali ya Tanzania na Visiwa vya Comoro zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo, elimu, afya, biashara na uwekezaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news