IGP Sirro afunga ukurasa wa madai ya Lissu, Lema

Jeshi la Polisi nchini limemtaka aliyekuwa mgombea urais wa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema warejee nchi kushiriki kujenga nchi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mkuu wa jeshi hilo, IGP Simon Sirro ameyasema hayo leo Novemba 19, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa wanahabari na IGP Sirro ulikuwa na lengo la kutoa tathmini baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020.

Amesema kuwa, kumekuwa na maneno kwamba kuna kutishiwa kwa viongozi wa kisiasa. "Mimi nimefanya juhudi kubwa sana hadi kuwaandikia barua viongozi wa CHADEMA wakati Tundu Lissu alipokwenda ubalozini,akisema anatishiwa. Niliwaandikia barua CHADEMA nikiwaomba Lissu aje Polisi atueleze anatishiwa na nani.

"Lakini waandishi wa habari unaweza kugombana na mtu yeyote akakutishia atakuua, hayo ni mambo ya kawaida, kama umetishiwa si unaleta taarifa Polisi? Hauleti taarifa Polisi unaenda kupeleka taarifa kwenye ubalozi, hivi nchi yetu imefikia hali hiyo kweli,"amesema IGP Sirro na kufafanua kuwa,hizo ni ajenda ambazo watu wametumia kwa ajili ya kuchafua nchi.

Pia amesema wakati wote wa kampeni Tundu Lissu alipewa ulinzi wa askari mwenye cheo cha Inspekta wa Polisi wa kuzunguka naye wakati wote wa kampeni na walimaliza vizuri kuzunguka kila kona ya nchi

IGP Sirro akizungumzia kuhusu madai ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, taarifa za Lema kutishiwa kuuawa hazina ukweli kwa sababu Polisi hawana taarifa yoyote.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi amesema kuwa, hakuna ripoti iliyopelekwa Polisi hivyo yeye anaona huo ni mpango mkakati, kwani kila mmoja anaweza kuchagua mpango mkakati wa kuishi katika maisha yake.

"Sisi kama Polisi wenye jukumu la kulinda watu na mali zao, hatuna taarifa zao za kutishiwa maisha kwa kiongozi yeyote, kwa hiyo nisema nchi yetu ipo vizuri na ina amani na utulivu na kama wameenda kwa ajili ya kupumzika, nawakaribisha warudi nchini, waje tufanye maendeleo ya nchi yetu, hakuna matishio, hakuna mtu aliye juu ya sheria,"amebainisha IGP Sirro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news