Rais Magufuli amuapisha Waziri Mkuu, Waziri Prof. Kabudi na Dkt.Mpango

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Novemba, 2020 amemuapisha Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mhe. Rais Magufuli pia amewaapisha Mawaziri 2 aliowateua hivi karibuni katika Baraza lake jipya la Mawaziri ambao ni Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi aliyeapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Dkt. Philip Isdor Mpango aliyeapishwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Hafla ya uapisho huo imefanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson.

Wengine ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Maspika Wastaafu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa Dini, viongozi wa Vyama vya Siasa pamoja na viongozi na watumishi wa Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali.



Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rais Magufuli amewataka Wabunge kutulia wakati akiendelea na mchakato wa uteuzi wa Mawaziri watakaunda Baraza la Mawaziri kwa kuwa ameamua kupitia kwa umakini mkubwa orodha ya Wabunge wote takribani 350 ili kupata wachache atakaowateua kuwa Mawaziri.

Mhe. Rais Magufuli ameeleza dhamira yake ya kutaka Serikali ifanye kazi zaidi katika kipindi chake cha pili cha uongozi kwa kuwa anatambua kuwa Watanzania wana imani na matumaini makubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho wamekichagua kwa ushindi mkubwa na wa kihistoria kwa Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo anataka viongozi ambao atawateua wawe na uwezo wa kweli wa kutimiza matarajio hayo ya wananchi.

Amebainisha kuwa kila kiongozi aliyeteuliwa atapaswa kufanya kazi kwelikweli vinginevyo atambue kuwa wadhifa alionao sio lazima afike nao mpaka mwisho wa Awamu hii ya Tano (yaani miaka 5) kwani uteuzi huo unaweza kutenguliwa na akateuliwa kiongozi mwingine.

Kwa upande wake, Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa imani kubwa aliyoionesha kwake na ameahidi kutekeleza wajibu wake kwa nguvu zaidi pamoja na kumshauri ipasavyo, na kwa kuanzia ameahidi kuchukua hatua mara moja dhidi ya upandishaji wa bei ya Saruji uliojitokeza siku chache zilizopita.

Halikadhalika, Mhe. Waziri Kabudi na Mhe. Waziri Mpango wameahidi kutekeleza wajibu wao kwa nguvu zaidi na kwa kugusa zaidi mahitaji ya wananchi, hasa baada ya kupata uzoefu wakati wakigombea katika majimbo ambako wamechaguliwa kuwa Wabunge katika uchaguzi mkuu uliopita

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news