Madiwani wote kupigwa msasa na wataalam wa Hombolo

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Joseph Nyamhanga amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanikisha upatikanaji wa fedha ili mafunzo elekezi yaweze kutolewa kwa madiwani wote katika halmashauri zote nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mhandisi Nyamhanga ameyasema hayo wakati akihutubia Mahafali ya 12 ya Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo Novemba 26, 2020 jijini Dodoma.

Amesema ili kuwe na ufanisi wa usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nafasi ya Chuo cha Serikali za Mitaa katika kutoa mafunzo ni kubwa ingawa kuna mafunzo ambayo yameandaliwa kutolewa kwa kutumia mfumo wa ujifunzani wa Kielektroniki (MUKI), lakini yanahitaji upatikanaji wa mtandao kwa maeneo mengi.

Hivyo, Mhandisi Nyamhanga ametoa wito kwa mamlaka za Serikali za Mitaa kufanikisha upatikanaji wa fedha ili mafunzo elekezi yaweze kutolewa kwa madiwani wote.

Pia amezitaka halmashauri kuangalia namna ya kuwapa kipaumbele wanafunzi wanaohitimu fani mbalimbali kupitia chuo hicho katika nafasi za ajira kwa sababu wahitimu hao ni wabobezi kwenye taaluma za Serikali za mitaa, hivyo wataleta ufanisi.

Aidha, ameupongeza uongozi wa chuo kwa kupata mafanikio ikiwemo upanuzi wa chuo, kuongeza udahili, ufaulu wa wanafunzi, kuongezeka kwa watumishi na mpango wa kuongeza wigo na ubora wa mafunzo.

“Napenda kuwapongeza kwa kufanikisha azima na tamanio la muda mrefu la kuanzisha Shahada ya kwanza ya Utawala na Menejimenti katika Serikali za Mitaa. Mafunzo ya Shahada ya kwanza yatakidhi mahitaji ya sasa ya kuboresha utoaji wa huduma na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Mamlaka za Serikali za Mitaa,"amesema Mhandisi Nyamhanga.

Pia Katibu Mkuu, Mhandisi Nyamhanga ametolea ufafanuzi changamoto za kimfumo, kisera na za kibajeti zinazokikabili chuo kuwa zimeshughulikiwa na zinaendelea kushughulikiwa kwa ngazi ya wizara.

Akiwasalisha hotuba ya Mkuu wa chuo, Dkt. Mpamila Madale amesema kwa mwaka wa fedha 2019/2020 chuo kilidahili wanafunzi 7,666 ikiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na mwaka 2007/08 chuo kilipoanza kutoa mafunzo ya muda mrefu kikiwa na wanafunzi 86 tu.

Akitaja mafanikio ya chuo kwa upande wa uboreshaji wa miundombinu, Dkt. Madale amesema kwa miaka mitatu mfululizo chuo kimejenga kumbi mbili zenye uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 504 kila moja kwa wakati mmoja na kumbi zingine mbili zenye kutumiwa na wanafunzi 250 na nyumba mbili za watumishi kupitia mfumo wa Force Account.

Wahitimu katika mahafali ya 12 katika Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo ni 5,752 na wamehitimu katika ngazi ya Astashahada ya Awali, Astashahada na Stashahada katika fani za Utawala katika Serikali za Mitaa, Uhasibu na Fedha katika Serikali za Mitaa, Menejimenti na Rasilimali watu, Maendeleo ya Jamii, Menejimenti ya Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu na Menejimenti ya Manunuzi na Ugavi.

Post a Comment

0 Comments