Makamu wa Pili wa Rais aahidi maboresho makubwa ZEC

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla amesema wakati watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wanapaswa kujipanga kwa ajili ya matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Serikali Kuu inajipanga kuwapatia jengo kubwa na la kisasa litakalokidhi mahitaji kwa watendaji wa taasisi hiyo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla ameema hayo wakati akizungumza na uongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar baada ya kufanya ziara fupi kwenye majengo yao yaliyopo Maisara na kuwapongeza kwa kusimamia Uchaguzi Mkuu uliomalizika kwa salama na amani.  
 
Amesema, Serikali pamoja na wananchi wameendelea kujenga imani kubwa kwa watendaji na viongozi wa Tume ya Uchaguzi kutokana na kazi ya kizalendo ya kuratibu uchaguzi iliyokwenda kwa umakini mkubwa jambo ambalo watendaji hao wanapaswa kupatiwa maeneo salama yatakayowapa utulivu wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Ipo haja kwa Serikali Kuu kuangalia watendaji wa Tume ya Uchaguzi wanapata jengo jipya na kubwa litakalokidhi mahitaji ya watumishi wake. Nafarajika kuona hatua ya kwanza ya upatikanaji wa eneo imeshakamilika,"amesisitiza Mtendaji Mkuu huyo wa shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Hemed Suleiman ameeleza kwamba, Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 umemalizika baada ya Tume ya Uchaguzi kusimamia Sheria na Miongozo iliyopelekea hata wale waliolalamika kutokana na zoezi hilo kutokuwa na sababu za msingi zinazoeleweka.


Amesema, watendaji wa Tume ya Uchaguzi wamesimamia vyema maamuzi ya wananchi jambo lililowapatia heshima kubwa na kuwapa faraja Wazanzibari walio wengi Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman amewahakikishia viongozi na watendaji wa tume hiyo kwamba Serikali itajitahidi kuchukuwa hatua za haraka katika kuona changamoto zilizowakabili zinapatiwa ufumbuzi unaostahiki.

Amesema, moja ya malengo ya Serikali Kuu ni kuendelea kujenga mazingira bora ya kazi kwa watumishi wa taasisi zake za umma ili yale mahitaji na huduma zinazostahiki zinawafikia wananchi mahali popote.

Mheshimiwa Hemed Suleiman amewakumbusha wananchi kwa vile Uchaguzi Mkuu tayari umemalizika hadi mwaka 2025 waendelee kuheshimu Sheria za nchi katika maisha yao ya kila siku ambayo yanaendelea kuwepo baada ya uchaguzi huo.

Akitoa taarifa fupi Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Thabit Idarous Faina amesema, elimu kwa ajili ya kupatiwa wapiga kura ambao ni wananchi bado itaendelea kuwa jukumu la Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo nchini.

Amesema, yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika siku chache zilizopita ikiwemo gharama za uchaguzi zilizokadiriwa kutumiwa shilingi bilioni 9.6 zilipungua na kutumika shilingi bilioni 6.5 tu na matokeo yake kunusuru shilingi bilioni 2.4.

Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi Zanzibar amesema kwamba, licha ya tume hiyo kuwa na matarajio ya kujenga Ofisi Kuu nyingine mpya lakini pia inaendelea kuimarisha ofisi zake zilizoko wilayani ili kupunguza usumbufu unaowakabili watendaji wake.

Amesema, Tume ya Uchaguzi hivi sasa inatumia baadhi ya majengo ya taasisi nyingine za umma kama ofisi zake ingawa tayari imeshafanikiwa kujenga majengo ya kudumu kwa ofisi zake za Wilaya ya Magharibi A Unguja na ile ya Micheweni Kaskazini Pemba.

Mkurugenzi Faina amefafanua changamoto ya gari inayokwaza utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za kila siku ambayo yameshachakaa baada ya kutumika kwa kipindi kirefu.

Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid amesema, moja ya siri kubwa ya taasisi hiyo inayosimamia uchaguzi inatokana na viongozi pamoja na watendaji wake kufanya kazi huku wakizingatia na kuheshimu maadili yao.

Mheshimiwa Hamid amesema, licha ya baadhi ya changamoto zinazowakabili viongozi na watendaji wa tume hiyo, lakini bado anafarajika kuona watumishi hao wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Amesema, katika kuona watumishi hao wanaendelea kuwajibika ipasavyo uongozi wa taasisi yake unajitahidi katika kuona kila fursa ikiwemo maslahi yao yanajengewa mazingira stahiki.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla ameanza ziara maalum ya kuzitembea taasisi na idara zilizo chini ya ofisi yake wiki moja tu baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali.

Post a Comment

0 Comments