Serikali kuimarisha Sekta ya Uvuvi iwe na tija zaidi

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekusudia ndani ya miaka mitano ijayo kuifanya Sekta ya Uvuvi kuwa na tija zaidi nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Rais Dkt.Magufuli ameyasema hayo leo Novemba 13, 2020 wakati akifungua Bunge la 12 na kulihutubia Taifa bungeni jijini Dodoma.
"Nchi yetu pia imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yanayofaa kwa shughuli za uvuvi, ikiwemo Ukanda wa Pwani, Maziwa, mito na mabwawa.

Hali hii inafanya sekta hii kuwa na nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza Pato la Taifa na pia kupambana na umasikini na tatizo la ajira.

Hata hivyo, kwa sasa, mchango wake bado ni mdogo. Hivyo basi, kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia kuikuza sekta hii, ikiwemo kuimarisha shughuli za uvuvi kwenye Bahari Kuu, ambako tumekuwa tukipoteza mapato mengi.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Shughuli za Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 2018; shughuli za uvuvi kwenye Bahari Kuu zinaweza kuingizia Serikali mapato ya moja kwa moja ya takriban shilingi bilioni 352.1 kwa mwaka endapo mifumo ya usimamizi na udhibiti ingekuwa imara na samaki wangechakatwa hapa nchini.

"Hata hivyo, mapato yaliyokuwa yamekusanywa kwa kipindi cha miaka tisa (2009 hadi 2017) yalikuwa shilingi bilioni 29.79, sawa na shilingi bilioni 3.3 kwa mwaka. Kiwango hiki cha mapato hakikubaliki.

Hii ndiyo sababu, tunataka, kwenye miaka mitano ijayo, kuisimamia vizuri shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu ili Taifa letu linufaike na rasilimali zake, kwa kuhusisha sekta binafsi. Kwa bahati nzuri, tayari, mwaka huu (2020) tumetunga Sheria Mpya ya Kusimamia na Kuendeleza ya Uvuvi wa Bahari Kuu.

Aidha, tumepanga kununua Meli 8 za Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika IFAD (4 upande wa Zanzibar na 4 upande wa Tanzania Bara) ili zishiriki katika uvuvi wa Bahari Kuu. Kama mnavyofahamu, suala la uvuvi wa bahari kuu ni la Muungano.

Tunakusudia pia kujenga Bandari kubwa ya Uvuvi itakayotoa ajira zipatazo 30,000; na tutaendelea kuihamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuchakata samaki.

Sambamba na kusimamia Bahari Kuu, tutakuza shughuli za uvuvi kwenye Maziwa yetu Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa) pamoja na Mito yetu mikubwa.

Tutahamasisha wavuvi wetu wadogo kujiunga kwenye vikundi ili tuweze kuwapatia mitaji, ujuzi, vifaa na zana za uvuvi; na halikadhalika tutapitia upya tozo na maeneo mbalimbali ili kuwapunguzia wavuvi kero na kuvutia uwekezaji.

Tutahamasisha pia watu binafsi kujenga mabwawa na kufuga kisasa kwa kutumia vizimba. Sekta ya uvuvi ni lazima itoe mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu. Wateule wote wa sekta hii ni lazima walisimamie hili,"amesema Rais Dkt.Magufuli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news