Miradi ya kimkakati Sekta ya Maji yadhamiria kutoa tabasamu vijijini, mijini

Kwa kutambua umuhimu wa huduma ya majisafi na salama kwa jamii, Serikali imeendelea kuwekeza kwenye miradi ya maji kote nchini kwa lengo la kuhakikisha huduma hiyo adimu inawafikia kwa haraka zaidi, anaripoti Mohamed Saif.
Uwekezaji huo ni pamoja na ujenzi wa miradi ya kimkakati ya kutoa maji katika maeneo yenye maji mengi na kuyapeleka kwenye maeneo yenye upungufu.

Hatua hii inawawezesha wananchi kujikita katika shughuli nyingine za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi katika kutafuta huduma ya maji.

Kwa maana nyingine ni kwamba Serikali inaendelea kutimiza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama ili kuondokana na sintofahamu za vikwazo mbalimbali wanavyokumbana navyo kwenye suala zima la huduma ya maji.

Takwimu za Wizara ya Maji zinaonesha kuwa wastani wa idadi ya watu wanaopata huduma ya majisafi na salama vijijini imeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.1 Machi mwaka 2020, na mijini hali ya upatikanaji wa huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2020.

Aidha, kwa mujibu wa maandiko mbalimbali ya kitaalamu yanayochapishwa kwenye Jarida la Diplomasia ya Maji Ulimwenguni na Habari za Kisayansi, watafiti kwa nyakati, maeneo na hadhira tofauti wanaweka bayana umuhimu wa maji kwa maendeleo ya jamii ambapo wanabainisha kwamba mahala penye uhakika wa majisafi na salama panakuwa na fursa nyingi zaidi za kiuchumi. 

Watafiti wanasema hali hiyo inageuka kuwa tofauti endapo huduma ya uhakika ya maji haipatikani.

Utafiti kupitia jarida hilo la kisayansi unaweza kuakisi na kudhihirishwa na wananchi wa kata ya Kikubiji, Wilayani Kwimba, Mkoani Mwanza ambao ni wanufaika wa mradi wa maji uliozinduliwa na Waziri wa Maji kwa wakati huo,Profesa Makame Mbarawa (Mb) Septemba 2019.

Ikiwa ni takribani miezi 15 hivi sasa tangu wananchi hao wa Kwimba waanze kunufaika na huduma ya maji, wanabainisha namna ambavyo mradi wa maji umeleta mabadiliko katika suala zima la kujiletea maendeleo, tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali kabla ya mradi.

Mzee Daniel Maganga (82), mkazi wa kijiji cha Shilima, Kata ya Kikubiji anasema tangu kuzaliwa kwake hajawahi kushuhudia maji ya bomba, lakini kupitia mradi huu wa maji ameshuhudia hilo na anaipongeza Serikali kwa kufanikisha huduma ya maji kwani kuyaona maji ya bomba nyumbani kwa umri wake ni kama ndoto.

Naye,Maria Mwanawile (42) anasema walitumia muda mrefu kufuata huduma ya maji, hali hiyo iliwasukuma kuamka mapema zaidi kabla jua halijawa kali kwenda kuchukua maji katika kijiji jirani cha Iselamagazi. Anasema kazi ya kufuata maji kwa jirani zao iliwapunguzia muda wa kufanya kazi nyingine za msingi katika makazi na za maendeleo.

Mwanawile anaongeza kuwa anahisi baadhi ya maradhi katika eneo lao yalichangiwa na matumizi ya maji ambayo siyo salama kwa baadhi ya wanajamii. Anafafanua kuwa baadhi ya wananchi walitumia maji katika eneo moja na mifugo, jambo ambalo sio salama kiafya kwa mujibu wa wataalamu.

“Tulikuwa tunatembea umbali mrefu,wakati mwingine unatuma watoto, kwa kweli haikuwa kazi nyepesi sana na kuna hatari kwani nakumbuka mwaka 2018 kulikuwa na tukio la watoto kuvamiwa na wahuni wakati wakienda kuchota maji,” Mwanawile anasema na kusisitiza mradi uliokamilishwa na Serikali ni mkombozi kwa makundi yote katika jamii yao, kuanzia watoto, vijana, hadi watu wazima.

Mkazi mwingine Alfred Lucas (32) anasema kupitia mradi huo wa maji Wilayani Kwimba anapata muda mwingi wa kufanya shughuli nyingine za kumuingizia kipato jambo ambalo lilikuwa gumu hapo awali.

Anasema kazi ya kuchota maji ilichukua muda mwingi zaidi hivyo kazi za kuingiza kipato katika shughuli za maendeleo muda wake kupungua na kipato kuwa kidogo.

“Kabla ya huu mradi tulikuwa tunagemea mabwawa ya maji ambayo siyo rasmi, wakati mwingine jua la kiangazi linayakausha, hivyo shughuli ya kutafuta maji ya mifugo na matumizi ya nyumbani inakuwa kubwa zaidi kwetu,” Lucas anasema na kuongeza kwa uchache kabla ya mradi wa maji maisha yalikuwa magumu,lakini kwa jambo lililofanywa na Serikali hivi sasa ni maendeleo tu, maji ya mifugo na matumizi ya nyumbani yapo ya kutosha, na shughuli nyingine zinaendelea.

Simulizi za wananchi hawa wakazi wa  Kikubiji zinadhihirisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inataka wananchi wajiletee maendeleo, na inawezesha mazingira ya kufanya hivyo. Serikali kufanikisha hilo ukweli unabaki kuwa huduma ya maji ndio kila kitu, maji ni chachu katika kuleta maendeleo, kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa lote.

Je, Rais Magufuli anasemaje? 

Katika hotuba yake ya kufungua rasmi Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Dodoma, tarehe 12 Novemba, 2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alizungumza kuhusu Sekta ya Maji na kubainisha kazi na mafanikio yaliyopatikana hususan kupitia miradi iliyoanza kutekelezwa chini ya uongozi wake.

“Kuhusu maji, mafanikio makubwa sana yamepatikana kwenye miaka mitano iliyopita. Tumetekeleza idadi ya miradi ipatayo 1,422 yenye thamani ya takriban shilingi trilioni 2.2,”  Rais Dkt.Magufuli anasema.

Hata hivyo, Rais Magufuli anasema wakati akiomba ridhaa ya wananchi kumchagua kwa kipindi cha pili,bado moja ya mrejesho wa wananchi haswa katika maeneo ya vijijini ilikuwa ni huduma ya maji. Wananchi wanahitaji huduma ya maji katika maeneo ambayo hawajafikiwa kikamilifu.

Rais Dkt. Magufuli anaelekeza watendaji katika Sekta ya Maji kuongeza jitihada na nguvu katika kufanyia kazi changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha zinazopelekwa vijijini kutekeleza miradi ya maji zinatumika vizuri na kwa mpango uliowekwa na Serikali.

“Nataka kuona miradi ya maji inayojengwa inakamilika kwa wakati; watendaji lazima wawe wabunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Mito na Maziwa yetu yatumike kikamilifu katika kuwafikishia huduma ya maji wananchi,” Rais Dkt. Magufuli alielekeza wakati akihutubia Bunge.

Aliliambia Bunge katika kipindi cha pili cha miaka mitano Serikali itaimarisha Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) ili kuupa uwezo mkubwa wa kifedha wa kutekeleza miradi.

“Tutakamilisha pia miradi mikubwa,ukiwemo wa Miji 28 utakaogharimu shilingi trilioni 1.2; Mradi wa Maji wa kutoa maji Ziwa Victoria unaogharimu takriban shilingi bilioni 600 na mradi mkubwa wa Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 520,” anabainisha Rais Dkt. Magufuli.

Hotuba inawataka wananchi kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji na miundombinu inayojengwa. Aidha, Rais Dkt. Magufuli anawaelekeza viongozi wote wakiwemo Wabunge, kulifanya suala la kutunza vyanzo vya maji na miundombinu yake kuwa ajenda muhimu katika shughuli zao za kila siku.

Je, mwitikio na utekelezaji ukoje?

Ni dhahiri kwamba suala la huduma ya maji kwa wananchi limepewa kipaumbele na Serikali. Baada ya hotuba ya Rais Dkt. Magufuli wakati akifungua Bunge la 12, ndani ya siku tatu Serikali ilisaini mkataba wenye thamani ya shilingi bilioni 70.5 na Mkandarasi kampuni ya ujenzi ya UNIK kutoka nchini Lesotho kwa ajili ya kandarasi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya Wilaya za Musoma vijijini na Butiama.

Utiaji saini wa mradi huo mkubwa wa maji ni wa kwanza kutekelezwa tangu kuanza kwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano.Ni moja ya ahadi za Serikali kutumia vyanzo vya maji vilivyopo katika kufikisha huduma ya maji ya kutosha kwa wananchi ili kuwawezesha kuongeza thamani ya shughuli wanazofanya kwa kutumia huduma ya maji na kukuza uchumi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,Mhandisi Anthony Sanga akizungumza wakati wa hafla hiyo alisema ujenzi wa mradi ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa wananchi wa Butiama na Musoma Vijijini na kwamba wizara anayoiongoza itahakikisha hakuna kikwazo kitakachochelewesha utekelezaji wa mradi.

“Wananchi wanausubiri kwa hamu kubwa mradi huu kama ambavyo walivyoahidiwa na viongozi wetu, sasa sisi kama Wizara ya Maji katika hili hatutokubali uzembe wa aina yoyote ile, tunachotaka ni kuona unakamilika kwa wakati na kwa ubora utakaoakisi thamani halisi ya fedha itakayotumika,” Mhandisi Sanga alisisitiza na kuwataka watendaji wa wizara yake kubaki Mkoani Mara ili kuhakikisha Mkandarasi anakabidhiwa eneo la ujenzi wa mradi ndani ya Saa 24 baada ya kusaini mkataba huo na kuanza kazi.

Mhandisi Sanga anabainisha kwamba fedha za utekelezaji wa miradi ya maji zinatoka kwa wakati na kwamba wizara anayoiongoza haitokuwa kikwazo katika kutimiza dhamira ya Rais Magufuli katika kuwafikishia wananchi huduma ya majisafi na salama.

“Mradi tuliosaini leo ni fedha za Serikali ya Tanzania; nina kila sababu ya kumshukuru Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea fedha hizi kwa ajili ya kuhakikisha mradi unajengwa, na nina ahidi sisi kama wizara hatutokuwa kikwazo, lazima mradi ukamilike kwa wakati,” Mhandisi Sanga alisema na kuongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa miezi 24, hata hivyo alimtaka mkandarasi kufanya kazi kwa saa 24 ili mradi ukamilike mapema zaidi.

Mhandisi Sanga kuwekea mkazo hilo anasema Serikali ya Awamu ya Tano ni ya vitendo na kwamba hakuna sababu ya mkandarasi yoyote kwenye miradi ya maji kutumia mwezi mzima kujipanga ili kutekeleza miradi.

Anaongeza kuwa inapofikia hatua ya kusaini mkataba ni lazima mkandarasi awe anaelewa kinachotakiwa kufanywa na kwamba maelekezo ya Serikali ni “kazi ianze na miradi ikamilike kwa wakati”.  

Mhandisi Sanga anasema wameamua kutumia utaratibu huo katika Sekta ya Maji ili kazi ziende haraka zaidi na kwa kiwango na ubora unaotakiwa na pia aliwakumbusha wananchi kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji kwa manufaa yao na kwa manufaa ya vizazi vijavyo. “Vyanzo vya maji lazima vilindwe ili kuwezesha miradi ya maji inayojengwa na Serikali kutoa huduma kwa wakati wote kwa wananchi bila kikwazo,” anasisitiza.

Tunashuhudia kazi kubwa imefanyika na shughuli ya kuwafikishia wananchi huduma ya majisafi na salama inaendelea. Endapo ingekuwa ni safari, basi ingeweza kusemwa kuwa umbali uliotumika kusafiri ni mrefu ila safari bado inaendelea.

Kwa muhtasari; maelekezo ya Rais. Dkt John Pombe Magufuli na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, bila kusahau ushuhuda wa baadhi ya wanufaika wa miradi ya maji, wananchi wa Kata ya Kikubiji ni kielelezo kinachojitosheleza kuainisha mwelekeo na dhamira ya Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wake kwa kuwafikishia huduma ya majisafi na salama kwenye makazi yao.

Kwa kutambua umuhimu wa majisafi na salama kwenye dhana nzima ya maendeleo endelevu na kuondokana na umasikini kwa jamii, Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025 inaweka bayana suala hili na tena kwa msisitizo wa kipekee kama nukuu kutoka kwenye Ilani hiyo inavyosomeka;

“Chama cha Mapinduzi kinatambua kuwa maji ni msingi wa uhai wa binadamu na injini ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Upatikanaji wa uhakika wa huduma ya majisafi na salama na usafi wa mazingira huchangia sana katika kuzuia magonjwa na hivyo kuimarisha afya na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla,” inaeleza Ilani ya CCM, Sura ya Tatu- Huduma za Jamii.

Hii yote inadhihirisha umuhimu wa majisafi na salama kwa mendeleo ya jamii na kwa namna ambavyo Serikali inavyotambua umuhimu huo na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa kuhakikisha kero ya maji nchini inakuwa historia.

Uwekezaji kwenye Sekta ya Maji unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni matunda ambayo watanzania wote watayafaidi kwa kuwa na huduma ya uhakika ya majisafi, salama na yenye kutosheleza wakati wote katika makazi yote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news