Prof.Msanjila asisitiza kuzingatiwa kwa Muongozo wa uendeshaji wa Rush

Imeelezwa kuwa, migogoro inayojitokeza kwenye Rush (Mlipuko wa Madini) inasababishwa na kjkundi kinachoteuliwa kusimamia uendeshaji wa Rush zinazoanzishwa katika maeneo mbalimbali,
anaripoti Issa Mtuwa (WM) Simiyu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila akifafanua na kutoa majibu ya hoja zilizotolewa na wachimbaji wadogo na wakulima wenye mashamba. Kulia kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Mmbaga na Oscar Kalowa. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Richard Abwao.

Hayo yamesemwa leo Novemba 23, 2020 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila alipotembelea kutatua mgogoro wa Rush ya Bulumbaka uliopo Bariadi mkoani Simiyu ambapo kuna mgogoro kati ya vikundi vya wachimbaji wadogo wa Mwananyanzala Mine Group, Umoja ni Nguvu, Ubunifu & Bulumbaka, Nyamagana Mine Group na Nguvu Moja Mine na mgogoro kati ya wachimbaji wadogo na wamiliki wa mashamba katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

"Rush ikitokea kikundi kilichoteuliwa kinatakiwa kizingatie miongozo, nini kifanyike kwa wakati gani. Mambo yanayo fanyika kwenye mgodi wanaosimamia wamepewa mamlaka ya kusimamia kwa niaba ya Tume ya Madini kwa kuzingatia miongozo,"amesema Prof. Msanjila. 

Amesema, migogoro inayojitokeza inahusu mvutano wa vikundi vya wachimbaji wadogo wakitaka kila kikundi kiwe msimamizi wa Rush, mgogoro mwingine huibuka kati ya wachimbaji na wamiliki wa mashamba ambayo madini yameibuliwa na mgogoro mwingine wa mgao unaotokea kati ya wachimbaji na wenye mashamba na mrahaba unaotolewa kwa serikali. Amesisitiza muongozo kuzingatiwa kwa kuwa kila kitu kinacholeta mgogoro umetoa maelekezo. 
Afisa Madini Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Oscar Kalowa, akisoma taarifa mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila katikati akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Simiyu ambapo baadhi hawapo pichani.
Wanakijiji waliokusanyika kumsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila aliyekuja kutatua mgogoro kwenye mgodi wa Bulumbaka

"Someni muongozo huu, unaonyesha kila kitu katika hayo mliyoyasema kila kitu kimewekwa wazi na ungefuatwa muongozo huu migogoro isingejitokeza,"ameongeza Prof. Msanjila.

Bwana Majuma Nzige ambae ni mchimbaji amesema chanzo cha mgogoro ni uongozi wa mgodi unaosimamia shughuli mgodini hapo. 

Ameongeza kuwa, hata asilimia 30 wanazotozwa hawaoni kitu kinachofanyika huku bwana Webiro Kihatala akisema, pamoja na kuwa na msimamizi, mazingira ya mgodi sio salama kwa maana mazingira ni machafu, hakuna vyoo, lakini pesa wanatoa. 

Kwa upande wa wamiliki wa mashamba, Ngila Machimu amesema mgogoro wao na wachimbaji wadogo wanachimba kwenye mashamba yao bila kupata faida na mazingira yao kwenye mashamba yanakuwa machafu kwa sababu hakuna vyoo.

Akijibu hoja zao kwa ujumla, Prof. Msanjila amesema suluhisho alilolisema ni uzingatiwaji wa muongozo na kutii. "Kila kilicholalamikiwa muongozo unatoa suluhisho,"amesema huku akisisitiza kwamba msimamizi atakayeteuliwa hapaswi kuwa mchimbaji katika eneo analosimamia na lazima atoke ndani ya mkoa wa Simiyu. 

"Naagiza mchakato wa kumpata msimamizi wa Rush hii, uanze upya na azingatie muongozo katika kutekeleza majukumu. Wakati tukisubiri msimamizi mpya huyu aliyopo ataendelea kusimamia ili kazi ziendelee,"amesema Prof. Msanjila.

Post a Comment

0 Comments