Serikali yawapongeza Zuchu, Nandy, Diamond kwa kutwaa tuzo AFRIMMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ndiye Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi ametoa pongezi na kongole kwa wasanii watatu wa muziki wa kizazi kipya Tanzania walioshinda Tuzo Mashuhuri za Muziki Duniani za African Music Magazine Awards (AFRIMMA) zilizotangazwa mjini jijini Dallas, Texas, Marekani. Anaripoti Mwandishi Diramakini.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Lorietha Laurence ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Dkt. Abbasi ametoa kongole kwa msanii Nassib Abdul maarufu "Diamond Platinumz" ambaye ameshinda Tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki, msanii Faustina Mfinanga maarufu Nandy (Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki) pamoja na Zuhura Othman maarufu Zuchu (Msanii Bora Anayechipukia Afrika).

"Tuzo hizi ni ishara ya wazi kwamba nchi yetu imesheheni johari zenye thamani na tuna magalacha wa kutosha katika mawanda ya muziki wa kizazi kipya.

"Serikali, kama anavyoahidi Mheshimiwa Rais katika hotuba zake, itaendelea kuwawekea mazingira bora wasanii wetu katika miaka hii mitano ili kuongeza ufanisi na mafanikio zaidi ya haya,"amesema Dkt.Abbasi.

Tuzo za AFRIMMA hutolewa kila mwaka ikiwa ni ushrikiano kati ya Taasisi ya AFRIMMA ya nchini Marekani na Umoja wa Afrika (AU), kuenzi kazi, vipaji na ubunifu katika uga wa sanaa Barani Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news