Viongozi Afrika wajitosa mzozo wa Ethiopia

Hatimaye viongozi wa nchi za Afrika wameanza juhudi za kutafuta suluhisho kwa mzozo unaozidi kuongezeka nchini Ethiopia, siku chache baada ya roketi kushambulia mji mkuu wa Eritrea na kuzusha hofu kwamba ugomvi huwenda ukaenea.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda Novemba 16, 2920 amekutana na Naibu Waziri Mkuu, ambae pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethopia, Demeke Mekonnen mjini Gulu, Kaskazini mwa Uganda, kuzungumzia hali ya huko Tigray.


Naye rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo anaelekea Addis Ababa katika juhudi za kuanzisha majadiliano.

Kwenye uwanja wa mapigano, serikali ya Ethiopia imetangaza jana kwamba ndege zake zimeshambulia vituo vya kijeshi kwenye mji mkuu wa Tigray wa Mekele baada ya kutangaza kwamba wanajeshi wa serikali wamekomboa miji kadhaa ikiwa ni pamoja na miji mkubwa ya Waja na Alamata.

Wakuu wa serikali ya Tigray wamethibitisha mashambulizi hayo na kudai kwamba mashambulizi ya ndege yalilenga maeneo ya raia. Katika hatua nyingine, Sudan imetoa wito kwa jumuia ya kimataifa kusaidia kukabiliana na wakimbizi wanaokimbia mapigano katika jimbo la Tigray wanaoingia mashariki mwa nchi.

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, limeripoti kwamba karibu wakimbizi 25, 000 walokuwa na njaa na kuchoka wameingia Sudan na kuonya uwezekano wa kuzuka janga la kibinadamu kwa sasa.

Post a Comment

0 Comments