Tanzania kuongoza kamati ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hati za Utambulisho ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, New York, kwa mwaka 2020/2021.

Uteuzi huu ulipendekezwa na Ofisi ya Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuidhinishwa kwa kauli moja na wajumbe wote wa kamati hiyo ambao ni 9.

Wajumbe hao ni Marekani, China, Urusi, Cameroon, Uruguay, Iceland, Papua New Guinea, na Trinidad na Tobago.


Novemba 23, 2020 Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Prof. Kennedy Gastorn, ameongoza kikao cha kwanza cha kamati hiyo kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa UNnews, hii ni mara ya kwanza Tanzania kushika nafasi ya kuongoza kamati hii nyeti ya Umoja wa Mataifa ambapo punde tu baada ya kuongoza kikao hicho.

Tarehe 15 mwezi Septemba mwaka huu wa 2020, baada ya pendekezo kutoka kwa Rais wa Baraza Kuu la 75 la Umoja wa Mataifa Volkan Bozkir, Tanzania iliteuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa mjumbe wa kamati hii.

Katika kikao cha jana chini ya uenyekiti wa Tanzania, Kamati imepitia hati zilizopokelewa za wawakilishi wa nchi wanachama na mashirika yenye hadhi ya uangalizi Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa Mkutano Mkuu wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Hii ni pamoja na Hati za wawakilishi watakaohudhuria (kwa njia ya mtandao) Mkutano Maalum wa 33 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 utakaofanyika kuanzia tarehe 3 had 4 Desemba 2020, kulingana na azimio namba 75/4 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mwenyekiti wa Kamati Balozi Gastorn anatarajia kutoa taarifa ya Kamati hii kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, siku ya Jumanne, 1 Disemba 2020.

Kimsingi, Kamati hii ina jukumu la kuzipitia hati zote za wawakilishi zitolewazo na Wakuu wa Nchi Wananchama au Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa, na kujiridhisha iwapo zimetimiza vigezo na masharti kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
 
Pia, nchi yoyote inaweza kupinga hati za wawakilishi wa nchi nyingine kwa kuleta hoja hiyo kwenye Kamati hii.

Mapendekezo ya Kamati katika mgogoro huo yanatakiwa kuridhiwa kwanza na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kupata nguvu ya kisheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news