Tanzania kuongoza Mkutano wa Saba wa Wataalamu wa Takwimu za Mazingira Duniani

Mkutano wa Saba wa Wataalamu wa Takwimu za Mazingira unaanza leo chini ya Uenyekiti wa Kaimu Mkurugezi wa Idara ya Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 10, 2020 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali,Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma.

Kaimu Mkurugezi wa Idara ya Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja. [Picha na DIRAMAKINI]

Mkutano huo wa siku kumi ambao unaanza leo Novemba 10 hadi 19 Novemba, 2020 utafanyika kwa njia ya mtandao na kuwashirikisha wataalamu wa takwimu za mazingira na masuala yanayohusiana nayo kutoka kanda zinazowakilisha wanachama wa Umoja wa Mataifa, taasisi za kimataifa na za kikanda.

Wajumbe wa mkutano huo ambao kwa mara ya kwanza uliitishwa mwaka 2014 watajadili mada mbalimbali zikiwemo Takwimu za Mabadiliko ya Tabianchi na Viashiria vyake, Ukusanyaji wa Takwimu za Mazingira, Kujenga Uwezo wa Kukusanya Takwimu za Mazingira na za Mabadiliko ya Tabianchi, Takwimu za Maji na Takwimu za Taka.

Madhumuni ya kuundwa kwa kamati hiyo ni kusaidia jukumu la Kamisheni ya Takwimu Umoja wa Mataifa (UNSED) la takwimu za mazingira katika kuweka viwango, mbinu na tafsiri ya takwimu za mazingira.Maeneo mengine ni pamoja na ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa takwimu za mazingira hasa za maji na taka pamoja na kusaidia kazi zinazohusiana na viashiria vya mazingira katika Malengo ya Dunia.

Post a Comment

0 Comments