TAKUKURU yang'ata walioomba 20,000/- mtoto apatiwe matibabu

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara leo Novemba 10, 2020 imewafikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Mtwara watuhumiwa wawili kwa kosa la kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuomba na kupokea rusha ya fedha kiasi cha shilingi 20,000, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Mtwara, Enock P. Ngailo amesema, watuhumiwa wametenda kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11, 2007 nchini.

Watuhumiwa hao ni Ashraz Dadi Likoma ambaye ni Afisa Tabibu, SDA Dispensary maarufu kama Zahanati ya Sabato, Mtwara na Fredrick Francis Mhongole ambaye ni mteknolojia mihonzi katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mtwara.

Kwa mujibu wa TAKUKURU, taarifa ilipokelewa kutoka kwa raia mwema Jumapili ya Novemba 8, 2020 majira ya saa tatu asubuhi akilalamika kuombwa rushwa ya shilingi 20,000 na Ashraz Dadi Likoma ambaye ni Afisa Tabibu katika Zahanati ya Sabato wakati alipohitaji kupata matibabu ya mwanaye aliyekuwa anaumwa.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Mtwara, Enock P. Ngailo amesema kuwa, Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mtwara inaendelea kutoa wito kwa wananchi wote mkoani humo kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

Ngailo amesema kuwa, wanapokuwa na taarifa za vitendo vya rushwa wazitoe katika taasisi hiyo katika ofisi iliyokaribu au kupiga simu namba ya dharura 113 au *113* na kufuata maelekezo. “Pia wanaweza kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 113 na huduma hii ni bure,”amesema Mkuu huyo wa TAKUKURU.

Post a Comment

0 Comments