Ujerumani yaichapa Ukraine 3-1 UEFA Nations League

Timu ya taifa ya Ujerumani imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ukraine katika pambano la mechi za ligi ya mataifa ya Ulaya Nations League usiku wa kuamkia leo ambapo bao la Ukraine limefungwa na Roman Yaremchuk dakika ya 12.
Mabao ya Ujerumani yalipachikwa wavuni na Leroy Sane na Timo Werner aliyefunga mabao mawili, kabumbu hilo safi lilichezwa Uwanja wa Red Bull Arena mjini Leipzig.

Katika mtanange huo kulikuwa na mashaka iwapo mechi hiyo ingechezwa baada ya wachezaji wanne wa Ukraine kupatikana na virusi vya corona baada ya kufanyiwa vipimo siku ya Ijumaa.

Wakati huo huo,timu ya taifa ya Uhispania ilitoka sare ya 1-1 na Switzerland katika mechi nyingine ya kundi hilo la D.

Kufuatia matokeo hayo, Ujerumani inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 9 ikifuatiwa na Uhispania yenye alama 8, Ukraine ni ya tatu ikiwa na alama 6 nayo Switzerland iko mkiani mwa kundi hilo ikiwa na alama 3.

Ujerumani itakutana na Uhispania siku ya Jumanne mjini Seville, huku timu zote zikiwania kumaliza ya kwanza katika kundi hilo.

Post a Comment

0 Comments