Ukuta unaozunguka machimbo ya Tanzanite waongezewa ulinzi wa kamera 306

Hatimaye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Madini chini ya Rais Dkt. John Magufuli imefanikisha kufunga mfumo wa CCTV kamera 306 kuzunguka mgodi wa madini ya Tanzanite uliopo Mjini Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila ameyabainisha hayo Novemba 17, 2020 wakati akipokea mradi huo wa kuimarisha usalama eneo tengefu la machimbo ya madini ya Tanzanite Mjini Mirerani kwa kutumia Mfumo wa Usalama wa CCTV kamera.
 
Ni katika ukuta na majengo yaliyopo katika mgodi pekee wa madini ya Tanzanite Mirerani, ambavyo vinafanya kazi nyakati zote za mvua, vumbi, baridi nyakati zote.

Profesa Msanjila aliyekua mgeni rasmi katika shughuli hiyo amesema, baada ya mradi wa ujenzi wa ukuta kukamilika na katika kuimarisha ulinzi kwenye eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani ilionekana kuna umuhimu mkubwa wa kuweka Mfumo wa CCTV Kamera kwa lengo la kugundua vitu na watu wanaoingia eneo ukuta.

Sambamba na kuhifadhi taarifa za kudumu, kuzuia wanaokusudia kufanya uhalifu na kufuatilia matukio yanayofanyika eneo la ukuta muda wote.

"Nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kwa miongozo makini anayotupatia katika kusimamia sekta ya madini ili kuhakikisha madini yetu yanawanufaisha watanzania.

"Ni wazi kuwa kiongozi wetu huyu amekua mstari wa mbele katika kutoa maelekezo yenye lengo la kuhakikisha kuwa madini yanaongezwa thamani hapa nchini,ushiriki wa watanzania katika uzalishaji na biashara ya madini unakua, wachimbaji wadogo wanaendelezwa na kuongezeka katika mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa,"amesema.

Amewataka wafanyakazi wa wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa umma, ambapo ametoa rai kwa wadau wote katika eneo hilo tengefu la Mirerani kujiepusha kabisa na vitendo vya rushwa ikiwemo utoroshaji madini.

Profesa Msanjila amesema, mwezi Februari, 2019 wizara ilialika makampuni sita kwa ajili ya kushiriki zabuni ya usambazaji na ufungaji wa mfumo wa kamera wa usalama katika ukuta wa migodi ya Tanzanite Mirerani ambapo wazabuni watano waliwasilisha gharama zao.

"Makampuni na watu mbalimbali walikuja wizarani na wengine waliletwa na taasisi za serikali kwa lengo la kutaka kupatiwa kazi ya kufunga mfumo wa CCTV kamera katika eneo hili la Mirerani, gharama walizowasilishwa zilikuwa kubwa sana, kwa mfano wapo waliowasilisha gharama ya sh.bilioni 83, bilioni 76, bilioni 33 na wengine bilioni 27.

"Lakini kama wizara tulichambua na kuona gharama hizo kuwa ni kubwa sana na kuamua kutowapatia kazi, ndipo tulipoipatia kazi kampuni ya Starfix Enterprises kwa gharama ya sh.bilioni 1.2,"amesema Profesa Msanjila.

Ameongeza kuwa, baada ya kufanyika na kukamilika kwa taratibu za manunuzi kampuni ya Starfix Enterprises ilikidhi vigezo vyote vya zabuni hiyo na kusainiana mkataba na wizara kwa kiasi cha sh.bilioni 1.2.

Mbali na kazi hiyo wizara imekamilisha ujenzi wa jengo la wafanyabiashara wa madini, jengo la kituo cha pamoja ndani ya ukuta wa Mirerani, uwekaji wa miundombinu ya umeme na taa kuzunguka ukuta umekamilika.

Amesema, ufungaji wa kamera za ulinzi kuzunguka eneo la ukuta wa migodi ya Tanzanite umekamilika na wameupokea mradi huo.

Amesema, vilevile ujenzi wa jengo la scanner, ufungaji wa scanner na kuweka mfumo wa Biometric entrace unatarajia kuanza muda si mrefu, "uwekezaji huu huu kwa pamoja unagharimu takribani kiasi cha sh.bilioni 4.2,"amesema.

"Lengo la hayo yote ni kuhakikisha kuwa shughuli zote zinazohusu biashara ya madini ya Tanzanite zinafanyika ndani ya ukuta, hatua hii inaimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi, kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite na kuongeza mapato ya serikali yatokanayo na madini ya Tanzanite,"amesema Profesa Msanjila.

Amesema, kufuatia ujenzi wa miundombinu hiyo, mapato ya serikali yameongezeka kabla ya ujenzi kutoka sh.milioni 238 kwa mwaka 2016-2017 hadi kufikia sh.bilioni 3.587 kwa mwaka 2018-2019 ambapo miundombinu hiyo imewezesha kupatikana mawe ya Tanzanite kutoka katika mgodi wa Bw. Saniniu Kurian Laizer ambayo yalivunja rekodi ya uzito duniani wa kilo 9.27, 5.103 na 6.33 yenye jumla ya thamani ya sh.bilioni 12.590,689,974.94 huku serikali ikijipatia mapato ya shilingi 919,120,368.17 kutoka malipo ya mrahaba, ada ya ukaguzi na ushuru.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news