Wafanyabiashara Tabora wakubaliana bei ya kuuza saruji

Uongozi wa Mkoa wa Tabora umekutana na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na saruji na kukubaliana faida wanayopata katika kila mfuko mmoja wanayouza isizidi shilingi 500 baada ya kuondoa gharama mbalimbali walizotumia ili kutowaumiza wananchi wanyonge, anaripoti Mwandishi Diramakini.
 
Wamefikia uamuzi huo katika mkutano ambao uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt.Philemon Sengati kwa lengo la kutafuta muafaka wa kutatua tatizo la bei ya saruji kupanda.

Akifungua mkutano huo Mkuu wa mkoa amesema, Serikali haikusudi kuwapanga bei elekezi ya saruji lakini wafanyabiashara wanalo jukumu la kuuza bidhaa hiyo kwa bei ambayo haitawafanya wananchi wanyonge washindwe kujenga na kuishi katika nyumba bora.

Dkt.Sengati amesema, kimsingi hakuna sababu ambazo zinazoweza kuhalalisha wafanyabiashara hao kupandisha saruji ambapo wapo wanauza shilingi 23,000 hadi 30,000 kwa mfuko mmoja wakati wao wananunua kiwandani kwa wastani unaoanzia 11,000 hadi shilingi 13,000 kwa mfuko mmoja.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Philemon Sengati (katikati) akizungumza na wafanyabiashara wa saruji kuhusu bei ya saruji mkoani Tabora.

Amesema, gharama za usafirishaji na posho za vibarua na madereva haiwezi kufanya bei ipande kwa kiasi hicho ambacho inawaumiza wananchi.

Dkt. Sengati amesema pamoja na kuwa sio jukumu la Serikali kupanga bei, lakini ina wajibu wa kuhakikisha bei za bidhaa zilizoko sokoni haziwaumizi wananchi wanyonge na kuwafanya wachukie Serikali yao

Amesema, wafanyabiashara ni wadau muhimu katika kushirikiana na Serikali kwenye shughuli za maendeleo ni vema wakahakikisha saruji inauzwa kwa bei nafuu ambayo haiwaumizi wananchi na kuwafanya wajisichie Serikali yao.

“Tumebaini wafanyabiashara wa rejareja wanauza saruji kwa shilingi 23,000 hadi 30,000 wakati bidhaa hizo amechukulia hapa hapa Tabora na hana gharama kubwa za kusafirisha mizigo, kitendo hicho ni kutaka kutengeneza fedha nyingi kwa kuwaumiza wanyonge, hakikubaliki, Serikali haiwezi kuvulimia,tutawachukulia hatua,"amesema.

Dkt.Sengati amesema, wafanyabiashara wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuungana na maono na mtazamo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambao unataka ubora na unafuu wa maisha kwa wananchi.

Mmiliki wa Kampuni ya Vimajo and Sons ambaye ni miongoni wa wanyabishara wakubwa wa saruji mkoani, Victor Chami amesema hivi sasa saruji inapatikana kwa shida na wakati mwingine wanalazimika kununua kwa wafanyabiashara wenzao ambao wana akiba na ndio maana ameongeza kiasi hicho kidogo.

Mfanyabiashara huyo ameongeza kuwa, hivi sasa wameamua kununua saruji aina ya Camel baada ya waliyokuwa wakinunua kwa wingi mkoani Tabora ya Dangote kutopatikana.

Amesema, wananunua saruji hiyo kwa gharama ya shilingi 13,340 kiwandani jijini Dar es Salaam na gharama za usafiri ni shilingi 5,000 na vibarua wa kushusha wanawalipa shilingi 100 na zinazobaki ndio faida yao.

Chami amesema kutokana na uhitaji mkubwa wa saruji hapa nchini kwa sababu ya miradi mikubwa inayojengwa na Serikali na mahitaji ya wananchi ni vema Seikali ikawabana wazalishaji wa saruji ili waongeza uzalishaji na waache kupeleka nje ya nchi.

Amesema, pindi Serikali itakapokamilisha miradi yake ndio wazalishaji waruhusiwe kupeleka nje ya Tanzania.

Chami amesema yeye atauza saruji kwa bei ya awali ya shilingi 18,500 kama ilivyokuwa kabla ya kuadimika kwa saruji mkoani humo.

Naye Beatus Massawe amesema ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa saruji mkoani ni vema kumuomba Dangote kuanzisha ghala kubwa Tabora kwa ajili ya mikoa ya Kanda ya Magharibi.

Amesema, kuwepo kwa ghala hilo litawasaidia kupata bidhaa hiyo kwa muda mfupi na gharama ambayo itawafanya wauze kwa bei ya chini kwa wananchi.

Massawe amesema, sanjari na hilo alimuomba Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora ili awasiliane na Shirika la Reli Tanzania liweze kuongeza mabehewa ya kuleta saruji kwa wingi mkoani Tabora.

Baada ya mkutano huo wafanyabiashara hao kwa pamoja wamekubaliana kuwa bei ya saruji aina ya Simba kwa rejareja iuzwe kwa shilingi 18,500 kwa mfuko, Dangote iuzwe kwa kiwango cha shilingi 19,000, Camel iuzwe kwa shilingi 19,500 na Nyati iuzwe kwa shilingi 20,000.

Walifikia uamuzi huo baada ya kujumulisha gharama kutoka uzalishaji kiwandani, za usafiri, posho ya vibarua na faida ya mawakala.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora amesema baada ya makubaliano hayo Serikali haitasita kuwachukulia hatua wafanyabiashara ambao watakutwa wanauza zaidi ya hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news