Wakulima, wafugaji Kiteto watakiwa kuthamini misaada ya Redcross

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Kanali Patrick Songea, amewataka wakulima na wafugaji kuthamini misaada iliyotolewa na Tanzania Redcross Society, anaripoti Mohamed Hamad (Diramakini) Kiteto.
Misaada hiyo ni mahindi na mbegu za majani pamoja na majani ya malisho ili kukabiliana na ukame ambapo mwaka huu mvua zitakuwa chache wilayani Kiteto.

Kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Kiteto itakuwa na mvua chache na chini ya wastani ambazo zitachangia ukame ambao jitihada zimeanza kukabiliana nao.

"Nawaasa wakulima na wafugaji Kiteto kazi hii iliyofanywa na Redcross na Jumuia za Kimataifa iwe na tija na tuwe na kitu cha kuwaonyesha. Mbegu hizi mlizopewa wakulima na wafugaji vyakula kwa ajili ya mifugo visaidie mifugo yenu kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa mmethamini msaada huu,"amesema DC Songea.

Amesema,pamoja na kuwepo kwa mashamba darasa katika eneo la mradi kuna kila sababu ya makundi hayo kuwa na utamaduni wa kubadilika kwa kutumia misaada hii.
Mratibu wa mradi wa usalama wa chakula Tanzania Redcross Society Kiteto, Haruni Mvungi akizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Kiteto amesema, mradi umezingatia malengo ya kushughulikia usalama wa chakula kutokana na athari za ukame pamoja na maafa.

Mvungi ametaja vijiji vinavyonufaika na mradi huo kuwa ni Orpopong, Ndaleta, Ndedo na Makame ambapo kaya 2,000 zimefikiwa kukabiliana na athari zitakazojitokeza.

Amesema kwa wafugaji mbali na vyakula vya mifugo walivyopewa watapatiwa elimu ya kuotesha malisho jambo ambalo hawakuwa na utamaduni na kujikuta wakipata madhara ya vifo vya mifugo yao kwa kuokosa malisho.

Mwenyekiti wa Tanzania Redcross Mkoa wa Manyara, Moses Basilla ameshukuru wafadhili wa mradi huo ambao ni American Redcross na IFRC, pamoja na uongozi wa Redcross Taifa.

Amesema utekelezaji wa mradi huu unafanyika kwa ushirikiano na Serikali ambapo wataalamu wa halmashauri wamekuwa wakitumika katika nyanja mbalimbali za utekelezaji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Makame Isaya Tutala amesema msaada huo umefika wakati mwafaka ambapo wafugaji wanahitaji chakula cha mufugo na pia mbegu za kupanda kwa malisho ya baadaye.

Post a Comment

0 Comments