DED Sunday Deogratius awapa somo watumishi wanaopangiwa kazi maeneo ya pembezoni

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa iliyopo mkoani Njombe, Sunday Deogratius amewataka watumishi mbalimbali wanaopangwa kufanya kazi hasa maeneo ya pembezoni mwa mji kutokimbia maeneo hayo kwani wanasababisha upungufu mkubwa wa watumishi ikiwemo kuwakosesha wananchi haki ya kupata huduma za msingi, anaripoti Damian Kunambi (Diramakini) Ludewa.
Hayo ameyasema baada ya kuona watumishi wengi wa wilaya hiyo kuomba kuhamishwa kwenda mijini kitu ambacho amesema hawezi kukubaliana nacho kwa kuwa kitapelekea kuwa na upungufu zaidi wa watumishi.

Amesema, mpaka sasa ofisini kwake mafaili yaliyowasilishwa kwake kutoka kwa watumishi hao zaidi ya asilimia 70 ni maombi ya uhamisho wa kwenda maeneo mengine ya mijini kitu ambacho kwa sasa hawezi kukiruhusu ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa, hali hii husababishwa  na wilaya hiyo kuwa moja ya wilaya zilizo pembezoni hivyo watumishi wengi hupendelea kufanya kazi mijini kuliko maeneo ambayo yako pembezoni.

“Nimekuwa nikipokea maombi mengi sana ya kuomba uhamisho lakini sijawahi kupokea maombi kutoka kwa watumishi wa maeneo mengine kuomba kuhamishiwa katika halmashauri yangu, hivyo kutokana na hali hiyo inaniwia vigumu kuruhusu watumishi waliopo katika wilaya hii kuhama kwakuwa nitakuwa na upungufu mkubwa wa watendani kwani hakutakuwa na wanaohamia kuja kushika nafasi zao,". amesema Deogratius.

Amesema, kuhama hama kwa watumishi hao kuna waathiri kwa sehemu kubwa kwani kunasababisha upungufu kwa watumishi hasa katika sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya.

Ameongeza kuwa, halmashauri hiyo inakabiliwa na upungufu wa walimu wa shule ya msingi 464 ambapo tayari wameshapeleka maombi tamisemi ya kupewa kipaumbele ili kupunguza ama kutatua tatizo hilo.

“Kuhama kwa walimu kunatuathiri sana. Maana ukiangalia baadhi ya shule za vijijini unakuta shule nzima ina walimu wawili mpaka wanne ambao wanatakiwa kufundisha darasa la kwanza hadi la saba kitu ambacho kinarudisha nyuma maendeleo ya elimu katika wilaya yetu,"amesema Deogratius.

Amesema katika sekta ya afya anaishukuru serikali kwa kuwa imekuwa ikiwaletea madaktari kila wanapoomba lakini changamoto iliyopo ni madaktari hao kutokubaliana na mazingira ambapo awali waliwaleta madaktari sita ambapo waliripoti madaktari wanne kati ya hao sita na hao wanne walioripoti wawili walikaa kwa muda mfupi na kuondoka na kupelekea kubakiwa na madaktari wawili. 

Ameongeza kuwa, hivi karibuni serikali imewaletea tena madaktari wanne ambapo nao imekuwa ni changamoto kwani mpaka sasa madaktari watatu kati ya hao wanne walioletwa wameondoka huku mmoja wao akiendelea na kazi.

Kutokana na hali hiyo mkurugenzi huyo ametoa wito kwa watu wote watakaoletwa kufanya kazi katika wilaya hiyo hasa katika sekta ya afya kuwa waje wafanye kazi kwani wilaya ya Ludewa iko vizuri na watapata motisha ya kutosha itakayowawezesha kufanya kazi katika mazingira mazuri.

“Nawakaribisha wale wote watakaoletwa kufanya kazi katika wilaya hii ya Ludewa kwani ni sehemu ambayo ni rafiki na salama ili waweze kuwahudumia wananchi kwakuwa serikali imewaamini na kuwaona kuwa wanafaa kuja kutumika katika wilaya hii kama ambavyo mimi nimeletwa kuwahudumia wananchi hawa na nimeweza hivyo naamini hakuna mwenye mapenzi mema atakayeshindwa kuja kutoa huduma huku,"amesema Deogratius.

Post a Comment

0 Comments