Rais Dkt.Mwinyi awapa faraja, nguvu mpya watumishi wa afya

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa wafanyakazi wa sekta ya afya wanajukumu kubwa la kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi (katikati) akifuatilia kwa makini changamoto zinazotolewa na wafanyakazi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika mkutano maalum na wafanyakazi hao uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abduulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar. Kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali pia Kaimu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe.Simai Mohamed Said (kushoto) Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Sera,Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dkt. Khalid Mohamed Suleiman. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Ameyasema hayo leo Desemba 31, 2020 wakati alipofany

a mazungumzo na wafanyakazi wa Wizara ya Afya kutoka kada mbalimbali, mazungumzo yaliyofanyia huko katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni jijini Zanzibar.

Amewataka wafanyakazi wa Wizara ya Afya kujitathmini wao wenywe kwanza hasa kwa kutoa lugha nzuri kwa wagonjwa kwani lugha nzuri ni nusu ya tiba.
Muuguzi na Mkunga, Rukia Balo kutoka Mpendae akiwasilisha mchango wake katika mkutano maalum wa Wafanyakazi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abduulwakil Kikwajuni cijini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi (hayupo pichani).

Amesisitiza umuhimu wa uongozi na kusema kwamba matatizo ya wafanyakazi yanaweza kutatulika iwapo viongozi watawajibika ipasavyo.

Amewataka wafanyakazi wa Wizara ya Afya hasa viongozi kubadilika na kufanya kazi kwa madhumuni ya kuimarisha sekta ya hiyo ikiwa ni pamoja na kujali haki za wafanyakazi wadogo.
Mchangiaji Hafidh Sheha Hassan katika kitengo cha maradhi ya Ngozi na maradhi ya kujamiiana akiwasilisha mchango wake katika Mkutano maalum wa Wafanyakazi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abduulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi (hayupo pichani).

Amewashukuru wafanyakazi wa sekta ya afya kwa kufanya kazi ngumu na katika mazingira magumu lakini bado wamekwua wakijitahidi huku akieleza kwamba bado kuna wafanyakazi wachache wanaomba rushwa na kutaka hali hiyo ichukuliwe hatua.

Sambamba na hayo amesema kuwa, wakati umefika wa kufikiria Bima ya Afya huku ikieleweka kwamba lengo si kufuta Sera ya Mapinduzi ya kutoa huduma za Afya bure bali kwa wale wenye kujiweza ni vyema wakawasaidia wasiojiweza na wale masikini waendelee kusaidiwa na serikali kwa kupitia mifuko ya Bima itakayoanzishwa.

Amewataka viongozi wote kukutana na wafanyakazi wao mara kwa mara jambo ambalo litawasaidia wafanyakazi kutokaa na matatizo vifuani mwao kwa muda mrefu, viongozi kutatua mambo ambayo yako katika uwezo wao na kuwataka wawajibike sambamba na kuwa wabunifu.

Katika suala zima la ugatuzi, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza haja ya kufanywa tathmini kuona kama kuna haja ya kuendelea mbele na mfumo huo kusimama hapo hapo ama kurudi nyuma kwani anaamini kwamba Zanzibar ni ndogo na inatawalika.

Aidha, ameeleza haja ya kuwepo kwa muundo wa utumishi ili watu waweze kulipwa vyema mishahara yao na kuitaka Wizara ya Afya kuharakisha jambo hilo linafanyika kwa azma ya kuwasaidia wafanyakazi hao.

Amesisitiza haja kwa kila mfanyakazi kutimiza wajibu wake na kuahidi kwamba yale yote yaliyokuwemo katika uwezo wa Serikali basi yatatekelezwa.Amesema kuwa, viongozi wana wajibu wa kuwasikiliza wananchi pamoja na wafanyakazi na kuwapongeza wafanyakazi hao kwa kuzungumza vizuri katika mkutano huo.

Dkt. Mwinyi ameahidi kwamba bado nafasi ipo ya kuzungumza nao kwani amedhamiria kufanya ziara katika maeneo yote yanayotolewa huduma za afya kwa lengo la kutafuta ufumbuzi na kusikiliza changamoto kwa upande wa Unguja na Pemba.

Amesema kuwa, kuna mambo matano muhimu yanayotakiwa kuwepo katika huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuwepo miundombinu mizuri ya afya na kueleza dhamira ya kweli ya kupata hospitali ya rufaa ya kisasa ambapo mipango hiyo ipo.

Amesema kuwa changamoto iliyonayo Serikali ya Awamu ya Nane ni kujenga hospitali hiyo ambapo hatua ambayo inafanyiwa kazi ambapo kwa kipindi cha mpito ipo haja ya kuweka mazingira mazuri katika hospitali ya MnaziMmoja angalau ikatoa huduma bora kwa wananchi.

Ameeleza haja ya kuwepo kwa wafanyakazi wakiwemo wataalamu na kueleza kwamba juhudi zitachukuliwa katika kuongeza wataalamu kwa kadri bajeti itakavyoruhusu.

Kuhusu vifaa, Dkt.Mwinyi amesema kuwa katika Wizara ya Afya kuna tatizo la matumizi ya fedha na mfumo mbaya wa utoaji wa dawa kutokana na kuwepo watu ambao hawawajibiki na kueleza kuwa hivi sasa ni wakati wa kuwatumbua wale wote wasiowajibika.

Aidha, ameeleza matumizi ya fedha na kusisitiza haja ya kuangalia mifumo ya kifedha katika Wizara hiyo huku akisema kuwa wale wanaotaka kutumia Bima ni vyema wakaruhusiwa.

Amesisitiza kwamba, kuna tatizo kubwa la uongozi katika Wizara ya Afya kuanzia juu hadi kwenye vituo ambapo watu hawawajibiki ipasavyo.

Amewataka wafanyakazi wote kutambua jukumu lao la kutoa huduma bora ambapo hatimae wananchi ndio watakaothitibisha mafanikio hayo huku akieleza haja kwa wafanyakazi hao kufanya kazi ili wapate haki zao. 

“Kuna wakati pesa zipo lakini mtu anaamua tu na anamwambia mfanyakazi sikupi…au kuna semina kila siku mtu huyo huyo ndie anaekwenda,”amesema Dkt.Mwinyi.

Sambamba na hayo amewashukuru wafanyakazi wote waliotoa huduma wakati lilipoporoka jengo la Beit el Ajaib hivi karibuni na kueleza jinsi alivyoridhika na huduma walizozitoa katika tukio hilo.

Rais amesema kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi wachache wanaiharibu kada hiyo ya afya na kueleza kwamba amesikia kilio cha wafanyakazi hao na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote waliyoyaeleza katika mkutano huo.

Nao wafanyakazi wa Wizara ya afya kutoka kada mbalimbali wameeleza changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa vifaa, fedha za kujikimu, posho, rasilimali watu, dawa, uongozi bora, mafunzo, mazingira ya kufanyia kazi na mambo mengineyo.

Aidha, wametoa shukurani kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa hatua yake hiyo aliyoichukua ya kwenda kuzungumza nao ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza changamoto walizonazo ambazo ameahizi kuzifanyia kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news