Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilivyoazimia kukomesha uvuvi haramu nchini

"Hatutavumilia jambo hili liendelee,Sisi kama wizara tumesema ni lazima tupate muarobaini wa uvuvi haramu, lakini na nyinyi wavuvi muwe tayari kutoa ushirikiano kwa serikali ili uvuvi haramu ukomeshwe mara moja," anasema Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul wakati akizungiumza na wavuvi wa Mkoa wa Manyara wakati wa ziara, anaripoti Mbaraka Kambona.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akisisitiza jambo kwa Mwakilishi wa Kampuni ya XIN SI LU, Suvi Zeng (hayupo pichani) alipotembelea eneo la ufugaji wa Samaki kwa kutumia Mabwawa la Kampuni hiyo lililopo Mkoani Manyara. Nyuma yake ni Viongozi wa Serikali pamoja na Wananchi waliojitokeza kumpokea Naibu Waziri huyo. (Picha na WMU/Diramakini).

Anawataka wanaojihusisha na uvuvi usiozingatia sheria na taratibu kuacha mara moja kwani Serikali haitakuwa na huruma kwa watakaokamatwa.

Waziri Gekul katika operesheni ya kupambana na uvuvi haramu iliyopita ilitumika karibu bilioni 1.2 jambo ambalo anasema halivumiliki na hivyo aliwataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa serikali ili kukomesha vitendo hivyo.

Anaongeza kwa kusema kuwa uvuvi haramu ukikomeshwa itasaidia kuokoa mazalia ya samaki na kuongeza idadi ya samaki katika maziwa na maeneo mengine.

Waziri Gekul anasema kuwa kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa viumbe maji kwa kutumia vizimba na mabwawa jambo ambalo anasema likisimamiwa vizuri litaongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umasikini na kuchochea uchumi wa taifa letu. 

“Niwaombe Wakurugenzi na viongozi wengine wa Halmashauri waangalie uwezekano kwenye zile asilimia kumi zinazotolewa na Serikali kwa vijana,wanawake na walemavu badala ya kuwapa mkononi wafanye utafiti ili kujua ujenzi wa mabwawa unagharimu kiasi gani ili wawajengee mabwawa ya kufugia samaki na tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira,” anasisitiza Gekul.

Kulipa kodi

Waziri Gekul anawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa uvuvi kuwafikia wavuvi wote na kuhakikisha wanalipia leseni za uvuvi ili kuzuia upotevu wa mapato na kukuza pato la Serikali.

“Hili litekelezwe haraka,kila mtu ajisikie vizuri kulipa kodi ya Serikali, lipeni kodi na mpatiwe risiti za mashine za elekroniki kwa kufanya hivyo kutazuia upotevu wa mapato ya serikali,” anafafanu.a

“Tutahakikisha wavuvi wote wanakuwa na leseni kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili lakini vilevile wale ambao hawana leseni waweze kukata leseni ili Serikali iweze kuwatambua na kupata mapato kupitia shughuli za uvuvi,” anasema Waziri Gekul.

Agizo kwa Wakurugenzi

Naibu Waziri Gekul anawataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutekeleza Waraka wa mwaka 2002 ambao unawataka kutenga asilimia 15 ya mapato yanayotokana na shughuli za Sekta ya Mifugo na Uvuvi na kuzirejesha kwenye sekta hizo ili kuboresha shughuli zake.

Anasema kuwa mwaka 2002 Serikali ilitoa waraka ambao unaelekeza kuwa Halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa mapato yanayopatikana kutokana na shughuli za sekta ya mifugo na uvuvi itengwe asilimia 15 na zirudishwe kwa sekta hizo ili kuboresha huduma kwa mifugo ikiwemo ukarabati wa majosho, minada na kununua chanjo za mifugo.

“Wakurugenzi rejeeni huo waraka ambao unadumu mpaka mwaka 2025 ili mtekeleze kama ulivyoagiza na tukifanya hivyo itasaidia kuboresha huduma za mifugo yetu na tupate mazao bora yanayotokana na mifugo hiyo,” anasema Gekul.

Anasema kuwa miundombinu mingi ya kuhudumia mifugo imechoka akitolea mfano minada ya kuuzia ng’ombe kuwa mingi haina uzio, mifugo inauzwa katika maeneo ya wazi jambo ambalo linachangia upotevu wa mapato ya Halmashauri.

“Najua katika Halmashauri zetu mara nyingi fedha huwa hazitoshi lakini ni muhimu kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha na tukifanya hivyo itakuwa rahisi kutenga hizo pesa ili kuboresha sekta za mifugo na uvuvi,hivyo naagiza baada ya kutoka hapa tukatekeleze hilo,” anasisitiza Gekul.

Waziri Gekul anasema kuwa muelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha majosho yanaboreshwa, minada inakarabatiwa na chanjo zinapatikana kwa urahisi ili wananchi wasihangaike kupata huduma kwa ajili ya mifugo yao.

Anawataka maafisa mifugo kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali ili kuzuia upotevu wa mapato kwani makusanyo yakiwa mazuri na huduma za mifugo zitaboreshwa.

Wawekezaji

Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo cha Eliya Food Overseas, Shabbir Virjee ameiomba Serikali kuona uwezekano wa kupitia upya na kupunguza kodi na tozo za mifugo ili waweze kushindana vyema katika soko la Kimataifa na nchi jirani kama Ethiopia, Kenya, Somalia na Uganda ambazo kodi zao ni ndogo na zinawawezesha kununua na kuuza mifugo pamoja na mazao yake kwa bei nzuri.

Akizungumza wakati waziri Gekul alipotembelea kuona shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho cha kuchakata mazao ya mifugo kilichopo katika Kijiji cha Namanga Mpakani, Wilayani Longido, Mkoani Arusha anasema kuwa kwa sasa wanalipa kodi zisizopungua tano kabla ya kusafirisha mazao ya mifugo nje ya nchi.

Anasema kuwa kutokana na jambo hilo limekuwa linawafanya wasiweze kushindana vizuri katika soko kwa sababu ya bei yao kuwa juu kutokana na kodi wanazolipia hapa nchini.

“Changamoto inayotukabili sisi ni kodi, tunalipa kodi zisizopungua 5, tunalipa kodi kwa Wizara ya kilimo shilingi 50 kwa kilo, Bodi ya Nyama tunalipa asilimia 1 ya thamani, Bakwata tunalipa kwa ajili ya kibali cha Halal.

"Tunalipa kodi kwa Vibali vingine, na tunalipa asilimia 0.1 ya kodi ya mionzi, kila hatua tunalipa kodi ambazo kusema ukweli zinatufanya tushindwe kushindana na nchi jirani ambazo kodi zao ni ndogo,” anasema Virjee

Anasema kuwa changamoto nyingine wanayokutana nayo ni kutopatikana kwa wanyama kama malighafi katika kiwanda hicho huku akiiomba serikali kuwasaidia ili waweze kupata Wanyama wengi ili kiwanda kiwe na uhakika wa malighafi. 

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kama hali itaendelea hivyo uendeshaji wa kiwanda hicho utakuwa mgumu kwa sababu watashindwa kushindana katika soko la ndani hata nje, huku akisema lengo la kiwanda hicho ni kutoa ajira kwa Watanzania wasiopungua 150. 

ATOA PONGEZI KWA WAWEKEZAJI

Waziri Gekul anawapongeza wawekezaji kwa jitihada kubwa wanazozifanya kuwekeza kwenye viwanda kwani vinatekeleza adhma ya Rais, Dkt.John Magufuli ya kuona Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na aliwahakikishia changamoto zao amezichukua na zitafanyiwa kazi.

“Nakuagiza Katibu Mkuu,Prof. Gabriel uunde timu itakayokuja kufuatilia ili kubaini hizo changamoto zote ikiwemo kwa nini Wafugaji wanapeleka mifugo yao kuuza nje ya nchi na taarifa hiyo itufikie haraka ili tuweze kuishauri Serikali kutatua changamoto hizo mapema,”anasema Gekul.

Pia, Waziri Gekul alimuagiza Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel kuangalia kwa namna gani Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inavyoweza kusaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa malighafi katika kiwanda hicho.

‘Hiki kiwanda ni lazima tukilinde, tufanye kila linalowezekana kukilinda kiwanda hiki, ikiwemo kutoa elimu kwa wafugaji kujua uwepo wa kiwanda hiki na faida zake, ili waweze kujua kumbe wanaweza kuuza ng’ombe wao hapa hapa nchini bila kukimbilia nchi nyingine,” anaongeza Gekul.

Aidha anasema Wizara itaendelea kuwawezesha wafugaji kupitia vituo vya uhimilishaji hapa nchini kuwapatia mbegu bora zitakazowasaidia kupata ng’ombe wazuri watakao wawezesha kupata kipato kizuri kupitia viwanda vinavyochakata mazao ya mifugo nchini. 

Tangu Kiwanda hicho kianze kufanya kazi miezi miwili iliyopita wameshachinja Mbuzi zaidi ya Elfu Saba (7000) na wameshaanza kupata masoko ya Kimataifa Uarabuni, Oman, Saudi Arabia na wanaendelea kufuatilia soko katika nchi ya China.

Post a Comment

0 Comments