Nahodha wa Ngorongoro Heroes amshukuru Dkt.Mabula kwa malezi bora

Nahodha wa Timu ya Taifa ya Vijana wenye Umri chini ya Miaka 20 (U-20) Ngorongoro Heroes, Kelvin John amemtembelea Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe Dkt Angeline Mabula ambae pia ni Mlezi wa Kituo cha Kuibua Vipaji, Kukuza na Kuviendeleza cha Football House kilichopo Bwiru jijini Mwanza.

Kituo ambacho alikuwa akikitumikia kabla ya kujiunga na Kituo chake kipya cha Brooke House College Football Academy kilichopo Mji wa Leicester nchini Uingereza, hivyo kumshukuru kwa mchango wake katika kukuza vipaji vya michezo mbalimbali ndani ya jimbo lake na nchi kwa ujumla.
Kelvin amemshukuru Mhe Dkt. Mabula kwa namna anavyojitoa pindi anaposhirikishwa changamoto zinazowakabili vijana kwenye sekta ya michezo kupitia kituo kilichokuwa kikimlea na hata mtu mmoja mmoja anapompelekea changamoto yake kupata msaada.

Sambamba na kumpongeza kwa kuendesha mashindano ya Ilemela Jimbo Cup ambayo yeye aliwahi kushiriki kabla ya kujiunga na timu ya taifa ya vijana.

"Ninamshukuru sana mama yangu Mhe Mabula kwa msaada wake kwetu sisi wana michezo, Ndio maana nilipopata fursa ya kuja mapumziko ya sikukuu ya Christmas nikaona nifike nizungumze nae mawili matatu,"amesema.

Aidha Nahodha Kelvin John amebainisha kuwa ipo tofauti kubwa sana ya aliposasa na hapo awali huku akiiasa Serikali na wadau kuwekeza katika michezo kwa kuhakikisha vifaa na mahitaji mengine yanapatikana kwa urahisi ili kusaidia vijana wenye ndoto ya kujiendeleza katika mpira wa miguu, na kuongeza kuwa Tanzania na Afrika ina uwezo mkubwa katika sekta ya michezo ukilinganisha na mataifa mengine duniani isipokuwa changamoto ya vifaa inachangia kurudisha nyuma ndoto za vijana wengi.

Nae Waziri Mhe Dkt. Angeline Mabula mbali na kupokea shukrani na pongezi zilizotolewa akamuasa nahodha huyo kuwa mzalendo kwa nchi yake sanjari na kuongeza juhudi kwa kutobweteka na mafanikio anayoyapata huku akishauri mamlaka za upangaji miji kutenga maeneo kwa ajili ya michezo na jamii kuyalinda maeneo hayo.

Akihitimisha msimamizi wa kituo cha Football House jijini Mwanza, Francis Fura Felician akasema kuwa Mbunge Angeline Mabula amekuwa akisaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazokabili kituo chao na amekuwa msaada mkubwa katika kutafuta vipaji, kuvikuza na kuviendeleza ili kufanya sekta hiyo kuwa rasmi na kuwa ajira kwa vijana waliowengi nchini wakiwemo Hussein Zuberi, Nasoro Mfaume, Agustino Athanas, Machumu Malagira, Adam Ramadhan na Michael Aloyce ambao wote walikuwa na nahodha wa timu ya taifa Kelvin John katika kituo hicho.

Post a Comment

0 Comments