TIC yatekeleza agizo la Rais Magufuli kutoa vibali kwa Wawekezaji ndani ya siku 14

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli la kutoa vibali kwa wawekezaji nchini ndani ya siku 14 ili kuvutia uwekezaji, anaripoti Jonas Kamaleki, Dodoma.
Utekelezaji huo umeanza kwa kuwakutanisha wakuu wa taasisi zinazojihusisha na huduma za utoaji vibali kwa wawekezaji chini ya Kituo cha Pamoja cha Uwekezaji (One Stop Facilitation Centre).

Miongoni mwao ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Leseni na Biashara (BRELA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ofisi ya Waziri Mkuu (Idara ya Kazi), Uhamiaji, TMDA, NEMC, TCU, TANESCO, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na TIC ambao ndiyo waratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 2,2020 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt. Maduhu Kazi amesema kuwa, kikao hicho kiliangalia namna bora ya kumrahisishia mwekezaji kupata vibali kati ya wiki moja na siku 10.

“Tumeamua kupunguza urasimu wa njoo kesho na tumeamua kuimarisha mifumo kwenye taasisi zetu ili isaidie kupunguza muda kutoa vibali,"amesema Dkt. Maduhu.

Ameongeza kuwa, TIC imelichukulia kwa uzito mkubwa takwa la kisheria la kutoa vibali ndani ya siku 14 kama Rais Magufuli alivyowaagiza.

Aidha, Dkt. Maduhu amesisitiza kuwa, mwekezaji hapaswi kuzungushwa bali anapaswa kuelekezwa nini cha kufanya kabla hajaleta maombi yake zikiwemo nyaraka muhimu anazopaswa kuwasilisha.

Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa, yapo maeneo ambayo yalikuwa yakichelewesha vibali na huduma nyingine kwa wawekezaji,maeneo hayo yameanishwa na yameanza kufanyiwa kazi ili huduma hizo zitolewe ndani ya siku 14.

“Sisi tumepata Mkuu wa nchi ambaye anataka kuona Sekta binafsi inakua kwa haraka kutoka hapa ilipo na kwenda juu zaidi kwa kiwango cha uwekezaji na ajira zinazopatikana,"amesema Dkt. Mhede.

Aliongeza kuwa elimu itatolewa kwa wawekezaji kuhusu wanayopaswa kufanya kabla ya kuwasilisha maombi na amesisitiza kuwa elimu hiyo itakuwa endelevu na hivyo kusaidia kutoa vibali kwa wakati kutokana na uwasilishaji wa nyaraka kamili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news