Aina mpya ya virusi vya Corona yazua taharuki Ulaya

Kituo kinachotoa taarifa za virusi vya Corona (COVID-19) cha Johns Hopkins kimeripoti mapema leo Januari 2, 2021 kuwa, kuna zaidi ya watu milioni 84 duniani wenye maambukizi ya virusi vya corona kwa sasa, anaripoti Mwandishi Diramakini (Mashirika).
Hopkins kimeeleza kuwa, Marekani inaendelea kuwa na maambukizi mengi zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote ambapo kuna zaidi ya maambukizi milioni 20, hii ikiwa robo ya maambukizi yote duniani. 

India ina idadi ya juu ikiwa ya pili kwa maambukizi ambapo kuna zaidi ya milioni 10, ikifuatiwa na Brazil ikiwa na maambukizi milioni 7.7. 

Maafisa wa afya wa Uingereza wameanza tena kutumia hospitali za dharura ambazo zilijengwa wakati janga lilipoanza huku nchi hiyo ikipambana kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi zaidi ya aina mpya ya virusi vya corona. 

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, wafanyakazi wa afya wanajiandaa kufungua tena hospitali za Nightingale za London iwapo ikutakuwa na haja ya kufanya hivyo. 

Hospitali za muda za Nightingale ziliwekwa na jeshi katika maeneo mbalimbali kuzunguka mji huo na ziliendelea kuwa tayari baada ya kutumika kidogo wakati wa wimbi la kwanza la maambukizi ya virusi vya corona. 

Januari 1, 2021, Serikali ya Uingereza ilirekodi maambukizi mapya 53,285 ya virusi vya Corona,jambo ambalo linatajwa si la kawaida.

Idadi hiyo ni ya chini kidogo ikilinganishwa na ile ya rekodi ya nyuma ya maambukizi 55, 892, lakini ni siku ya nne leo kuwa, maambukizi mapya yamevuka 50,000.Hiyo ni karibu mara mbili ya idadi ya kila siku katika wiki chache zilizopita. 

Maafisa wa afya wa Uingereza wanasema ongezeko la kesi mpya la maambukizi yanayotokana na aina mpya ya virusi vya corona, vilivyogundulika Uingereza, ambayo ina maambukizi zaidi. 

Aina hiyo mpya imepelekea watu kuzuiliwa tena kutotoka nje nchini Uingereza na masharti ya kusafiri kwa wasafiri kutoka Uingereza. 

Gazeti la New York Times limeripoti kuwa, nchi 33 hivi sasa zimethibitisha aina mpya ya virusi vya corona na zaidi ya nchi 40 zimezuia wasafiri kuingia nchini kutoka Uingereza. 

Uturuki imekuwa ni nchi ya karibuni kuanzia Januari Mosi, 2021 kupiga marufuku Waingereza kuingia nchini humo baada ya kugundua maambukizi 15 ya aina mpya ya virusi vya corona. Uturuki imesema maambukizi hayo yote mapya ni ya wasafiri waliowasili kutoka Uingereza. 

Serikali ya Ufilipino inasema itapiga marufuku kuingia wasafari wa kigeni kutoka Marekani baada ya aina mpya ya virusi vya corona kuthibitishwa huko Florida. Maafisa wanasema katazo hilo litaendelea hadi Januari 15, 2021. 

Florida ni jimbo la tatu Marekani kuthibitisha kuwepo kwa aina mpya ya virusi vya corona baada ya Colorado na California. 

Ufaransa ina maambukizi ya juu zaidi ya COVID-19 Ulaya Magharibi ambapo kuna zaidi ya watu milioni 2.6 walioambukizwa, kwa mujibu wa Hopkins. 

Ufaransa imepeleka zaidi ya polisi 100,000 kuzuia sherehe za mwisho wa mwaka, lakini wapenzi wa tafrija Kaskazini Magharibi mwa Ufaransa, karibu na Rennes walitayarisha mkusanyiko mkubwa kinyume cha sheria. 

Kwa mujibu wa The New York Times, polisi walikuwa wamepelekwa katika eneo hilo kutawanya mkusanyiko huo, lakini walikabiliwa na upinzani wakati washeherekeaji hao walipoanza kuwatupia chupa na mawe maafisa wa polisi na kuchoma gari moja ya polisi.

Wakati huo huo, Serikali ya Ireland imesema jana ilikuwa imetoa taarifa zisizo kamili juu ya maambukizi ya virusi vya corona katika siku za karibuni kwa idadi iliyo pungufu ya zaidi ya maambukizi 9,000, wakati mfumo wa kutoa taarifa ulipokuwa una matatizo. Nchi hiyo iliripoti maambukizi 1,754 yaliyothibitishwa jana. 

Aidha, Italia imeripoti vifo 462 vinavyotokana na aina mpya ya virusi jana. Nchi hiyo ina idadi kubwa zaidi ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona Ulaya ikiwa ni zaidi ya vifo 74,600 kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Nchini China, viwanja viwili vikuu vya ndege upande wa Kaskazini Mashariki vinawataka wasafiri wanaondoka kuonyesha uthibitisho wa vipimo vyao kuwa hawana maambukizi kabla ya kupanda ndege. 

Utaratibu mpya katika viwanja vya ndege vya Shenyang na Dalian umekuja wakati nchi hiyo ikichukua hatua kuzuia mlipuko mdog,o lakini sugu ya maambukizi ya COVID-19 Kaskazini mwa mji mkuu, Beijing na imeripoti maambukizi 19 ya aina mpya ya virusi.

Post a Comment

0 Comments