DC Dkt.Naano aokoa maisha ya vijana waliodaiwa kupora fedha

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt.Vincent Anney Naano amelazimika kuokoa maisha ya watu wawili wanaodaiwa kumpora kijana mmoja Shilingi Milioni 1.8 waliokuwa wakipigwa na wananchi wenye hasira kali baada ya kuwakamata watu hao, ambapo gari lake limetumika kuwabeba na kuwapeleka polisi na yeye kusitisha majukumu yake kwa muda kuokoa maisha yao, anaripoti Amos Lufungilo (Diramakini) Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt.Vincent Naano kushoto mwenye suti nyeusi akiwazuia wananchi wasiwapige eatu waliowakamata kwa madai ya wizi waliokaa chini.(Picha na Amos Lufungilo/Diramakini).

Tukio hilo limetokea leo Januari 16, 2021 majira ya saa tano na nusu za asubuhi jirani na Kanisa la Angilikana  lililopo Manispaa ya Musoma jirani na Ofisi za Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, ambapo watu hao baada ya kumpora kiasi hicho cha fedha maeneo ya Mwigobero walichukua usafiri wa bodaboda na kumwambia awapeleke eneo la Majitarodi wakidai wanaharaka na safari wakamwelekeza wapite njia ya Uwanja wa Karume nyume ya kiwanja cha Ndege cha Musoma.

Mwendesha bodaboda wakati akiendelea na safari ya kuwapeleka, aliona pikipiki mbili zikimfuatilia kwa kasi nyuma, huku kati ya pikipiki hizo mojawapo ilikuwa imembeba kijana waliyemuibia, na ndipo walipomwambia aliyewabeba aongeze kasi na yeye akashituka na kupunguza mwendo akiwauliza mbona nyuma tunafukuzwa, na ndipo mmoja wao akashuka kwenye Pikipiki hiyo na kutupa kiasi cha fedha alizokuwa nazo na kuanza kukimbia wakiwa wamefika eneo jirani na Kanisa la Angilikana jirani pia na Makao makuu CCM Mkoa wa Mara.

Kufuatia yowe zilizokuwa zikipigwa na watu kujitokeza kwa wingi kumfukuza mtu huyo zilizaa matunda, na kumkamata na kuweza kumuunganisha na mwenzake ambaye pia alishuka kwenye bodaboda waliyokuwa wameikodi kwa madai kwamba, wanasafiri na ndipo walipoanza kupewa kipigo huku wakiulizwa na wananchi kwa nini wanafanya kazi haramu ya kuibia watu.

Umati huo wa Wananchi ukiwa bado unawapa kipigona kuwahoji huku baadhi yao wakiwa na jazba wamebeba mawe ghafla mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt.Vincent Naano alijitokeza ambapo alikuwa katika majukumu ya kiserikali alikutana na kadhia hiyo eneo hilo na akashuka ndani ya gari lake kwenda kuwazuia wananchi wasijichukue hatua mkononi na ndipo alipowahoji na wakakiri kumwibia kijana huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt.Vincent Naano mwenye suti nyeusi aliyesimama akishuhudia watu wawili wakipakiwa ndani ya gari lake kuwanunusuru dhidi ya kipigo Kutoka kwa wananchi kwa madai ya kumuibia kijana sh.milioni 1.8. (Picha na Amos Lufungilo/Diramakini).

Kwa upande wake kijana huyo ambaye (jina lake halikufahamika) amesema alikuwa na kiasi Cha shilingi Milioni 1.8 akitokea Kijiji cha Gabimori Wilaya ya Rorya akipeleka fedha hizo jijini Mwanza kwa baba yake, ambapo baada ya kushuka ndani ya feri inayofanya safari zake Kinesi Rorya - Musoma eneo la Mwigobero watu hao walimuita na kumuuliza anakokwenda wakimzongazonga na ndipo walipochukua fedha hizo mfukoni mwake kwa nguvu na kuchukua usafiri wa bodaboda na yeye akalazimika kukodi bodaboda kuwafukuza kwa nyuma.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma amelazimika kuwaambia baadhi ya wananchi waliokuwa eneo la tukio, wawapakie ndani ya gari lake pamoja na Kijana waliyemuibia na wawapeleke Polisi haraka, ambapo mmoja kati yao alikuwa akitokwa na damu kufuatia majeraha aliyekuwa ameyapata kutoka kwa wananchi hao, ambao wengi wao walikuwa ni waendesha pikipiki huku wakilizonga gari hilo wakitaka washushwe wawaua kwa madai kwamba, watu hao wanarudisha nyuma maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla.

"Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya watu hawa ungetuachia tuwaue kwa sababu wamechagua kazi hii na malipo yao ni kifo waliyemwibia yupo hapa, na wamekiri, na hela wanazo ushahidi wote upo, watu kama hawa hawafai kabisa kuishi duniani wakushukuru sana wewe vinginevyo walikuwa wetu,"alisikika dereva bodaboda ambaye alikuwa akilizonga gari la Mkuu wa Wilaya wakati likiwapeleka polisi.

Akizungumza na wanahabari waliofika eneo la tukio hilo, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wa wananchi wa Wilaya hiy, kuachana na tabia ya kujichukulia Sheria mkononi, bali wanapowakamata wezi wawapeleke Polisi kwa ajili ya kuwajibishwa na Sheria kwani Nchi hii inaongozwa na Sheria.

"Niwashukuru Wananchi kuwafukuza na kuwakamata watu hawa, lakini niombe wanapokamata wezi wapige simu Polisi ama Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na siyo kujichukulia hatua mkononi Kama ambavyo walikuwa wanafanza kwa watu hawa waliowakamata," amesema Dkt. Vincent Naano.

Post a Comment

0 Comments