Mahusiano yataka kuondoa uhai wa binti kwa kuchangaya pombe na sumu

Secilia Ching’unyau (22) mkazi wa Magoweko wilayani Gairo Mkoa wa Morogoro amejaribu kujiua kwa kunywa sumu ya kuhifadhia mahindi aliyoichanganya na pombe aina ya vodka-cuca, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Uamuzi huo ameuchukua kwa madai ya wazazi kuingilia kuvunja mahusiano kati yake na mpenzi wake.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, SACP Fortunatus Muslim amesema, tukio hilo limetokea majira ya saa moja usiku katika mtaa wa Magoweko Tarafa na Wilaya ya Gairo, ambapo alijaribu kujiua kwa kunywa sumu ya kuhifadhia mahindi aina ya Acteric.

Amesema,chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi bada ya wazazi kuingilia kuvunja mahusiano na mpenzi wake.

Amesema, inaelezwa mtuhumiwa alikunywa sumu hiyo kwa kuchanganya na pombe aina ya vodka-cuca, ambapo alikutwa amelewa na kupoteza kumbukumbu huku akiwa ameegemea ukuta wa nyumba na pembeni yake kukiwa na vikopo viwili vya pombe aina ya vodka-cuca vikiwa vimeshatumika na vikopo viwili vyenye kuhifadhia mahindi aina ya acteric ambavyo vilikuwa bado havijatumika.

Kamanda Muslim amesema mtuhumiwa amelazwa katika Kituo cha afya Gairo akiendelea na matibabu na kwamba hali yake inaendelea vizuri huku taratibu zingine kwa ajili ya hatua zaidi zikiendelea.

Post a Comment

0 Comments