Watoto Milioni 1.5 waandikishwa kuanza darasa la kwanza 2021

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa naSerikali za Mitaa (TAMISEMI) imetangaza kuwa takribani watoto milioni 1.5 wameandikishwa kuanza darasa la kwanza kwa mwaka 2021,anaripoti Nteghenjwa Hosseah (OR-TAMISEMI).
Naibu Katibu Mkuu wa Tamiseni anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli ameyasema hayo aliopozungumza kuhusu shule za msingi na sekondari zilivyojipanga kuwapokea wanafunzi walioanza masomo yao ya darasa la kwanza na kidato cha kwanza.

Mweli amesema idadi hiyo inaweza kuongezeka baada ya siku kadhaa kadri ambavyo watoto wengine watakavyoendelea kuandikishwa.

Wakati huo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Seleman Jafo,amesema shule za msingi na Sekondari zimejiandaa vyema kuwapokea wanafunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza na masomo yamekwishaanza mwanzoni mwa juma hili.

Waziri Jafo amesema hatua hiyo hatua hiyo inatokana na uwepo wa miundombinu ya uhakika wa madarasa katika shule zilizopo katika halmashauri zote nchini kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa na wa kidato cha kwanza waliochaguliwa kuingia shuleni.

Amesema kwa utaratibu uliopo hadi hivi sasa, watoto wapatao 759,737 sawa na asilimia 81.4 waliofaulu na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wameanza masomo yao nchi nzima huku wanafunzi 78116 waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza wakisubiri awamu ya pili.

“Nimefanya ziara ya kukagua miundombinu iliyopo katika shule mbalimbali takribani mikoa 14 nchini na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa inayoendelea katika baadhi ya maeneo, kikubwa nisisitize kuwa shule zote zipo tayari kuwapokea wanafunzi hao,"amesema Jafo.

Akitolea mfano wa Mkoa wa Kagera, Jafo amesema kutokana na miundombinu ya vyumba vya madarasa iliyojengwa mkoani humo, kuna uhakika wa asilimia mia moja kwa wanafunzi wote wa kidato cha kwanza pamoja na wale wa darasa la kwanza wanaoendelea kuandikishwa kuanza masomo yao kuanzia bila uwepo wa hata mmoja atakayekosa nafasi.

Amesema kwa mkoa wa Dar es Salaam, tayari kuna uhakika wa wanafunzi 14926 wa kidato cha kwanza waliotarajiwa kukosa nafasi ya kuingia kidato cha kwanza kwa sababu ya ukosefu wa madarasa, wataripoti shule kama kawaida kutokana na mkoa huo kuweka mkazo katika ujenzi wa vyumba vilivyokuwa vikihitajika.

Waziri Jafo amesema ujenzi huo wa vyumba vya madarasa unaofanywa katika Halmashauri zote nchini umetokana na maagizo mbalimbali yaliyotolewa kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuhakikisha miundombinu ya madarasa hayo inajengwa kwa kasi ili kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madara uliokuwepo.

Walimu Wapya

Aidha Waziri Jafo aliwaagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatoa fedha za kujikimu kwa walimu wapya walioripoti katika shule mbalimbali zilizopo katika halmashauri zao ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Alisema walimu hao wanapaswa kupewa fedha hizo mara wanaporipoti katika shule walizopangiwa na kwamba kitendo cha kuwachelewesha kuwapatia fedha hizo hakikubaliki kwa kuwa wao ni binadamu na wana mahitaji yao muhimu ya kila siku.

Agizo kwa Halmashauri

Alizitaka kuhakikisha zinakamilisha ujenzi wa miundombinu ya madarasa katika maeneo ambayo bado hawajatekeleza hivyo na huku akisisitiza kuwa matarajio ni kuona ifikapo Februai 28 Mwaka huu kila mwanafunzi aliyepaswa kuwa darasani awe darasani akiendelea na masomo yake kama ilivyopangwa.

Naibu Katibu Mkuu Tamisemi

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa (Tamisemi-Elimu) Gerald Mweli, aliwataka wazazi ambao watoto wao wamefikia umri wa kuandikisha kuanza darasa la kwanza kuhakikisha wanakwenda na kuwaandikisha ili waweze kuanza masomo yao. 

Alisema kitendo cha wazazi hao kuendelea kuwaacha mitaani watoto ambao umri wao umetimia kuanza shule ni kinyume cha sheria na zaidi kinawanyima haki zao watoto hao.

“Serikali imeweka utaratibu wa elimu bure kwa kila mwanafunzi, hivyo kwa watoto wanaopaswa kuingia kidato cha kwanza wamepelekwe na kuanza masomo yao, lakini kwa wale wanaopaswa kuandikishwa darasa la kwanza ni vyema kwa wazazi kuwapeleka ili waweze kuanza shule” alisisitiza Mweli.

Alimaliza kwa kusema kuwa hana shaka na ujenzi wa miundombinu ya madarasa uliofanywa katika mikoa yote kutokana na kujiridhisha na ziara aliyoifanya katika mikoa mbalimbali kuangalia utekelezaji wake.

Post a Comment

0 Comments