Waziri Jafo atoa siku 14 takwimu za watoto wenye mahitaji maalum zipatikane

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo amewaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanasimamia ipasavyo utaratibu wa kubaini watoto wenye mahitaji maalumu,anaripoti Atley Kuni, (Mwanza).
Utaratibu wa kubaini watoto wenye mahitaji maalum utafanyika kwa muda wa siku 14 kuanzia Januari 7 hadi 21, 2021.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo jijini Mwanza alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wataalam wa elimu maalum, maafisa maendeleo ya jamii na wauguzi, yanayofanyika katika ikumbi wa Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza.

“ Baada ya mafunzo haya kuanzia tarehe 7 mpaka 21 Januari mwaka huu tutafanya kampeni ya kubainisha watoto wote wenye mahitaji maalum. Niwaagize wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kila mmoja akasimame kidete tufanikishe utaratibu huu,”amesema Mhe.Jafo.

Waziri Jafo ameongeza kuwa, “kukamilika kwa utaratibu wa kutambua watoto wenye mahitaji maalum itakuwa suluhu yakubainisha mahitaji maalum kwa watoto wenye mahitaji maalum hususani eneo la miundombinu ya shule.”
Aidha, Waziri Jafo amewataka pia viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji, kuwa vinara katika kubainisha watoto wenye mahitaji maalum katika maeneo yao.

“ Viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji ndio mnaoishi na jamii kwa karibu katika mitaa yenu na pia ndio wanaojua nyumba ya mwanachi gani kuna mtoto mwenye mahitaji maalum, hivyo mnatakiwa kutoa ushirikiano wakutosha kwa wataalam hawa watakapofika kutekeleza kazi hii.”

Waziri Jafo pia amemuagiza Mkurugenzi wa Elimu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kuhakikisha anawasilisha taarifa ya takwimu sahihi katika Ofisi yake mara tu baada ya kukamilika kwa kazi hiyo ambayo inakwenda sambamba na upangaji wa mipango ya maendeleo ya nchi.

Awali akitoa salaamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella, alimhakikishia Mhe. Waziri kuwa, kazi hiyo itafanyika ipasavyo.

“ Kwa niaba ya wakuu wa mikoa wenzangu, nikuhakikishie kazi hii ifanyike ipasavyo na pia tutasimamia kwa umakini mkubwa ili tija iliyo kusudiwa na Serekali iweze kutimia,"amesema.

Jumla ya wataalam 314, kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara wanapatiwa mafunzo ya siku tatu katika Chuo cha Ualimu cha Butimba, kilichopo mkoani Mwanza, mafunzo hayo yanashabaha ya utekelezaji wa sensa maalum ya kubaini watoto wote wenye mahitaji maalum ili waweze kuandikishwa na kuanza masomo katika shule mbalimbali nchini.

Post a Comment

0 Comments