Italia yautaka Umoja wa Mataifa kuchunguza mauaji ya Balozi wao DRC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Luigi Di Maio amesema kuwa ameuomba Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi juu ya shambulizi lililomuua balozi wake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Luca Attanasio, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Waziri Mkuu wa Italia,Mario Draghi akigusa moja ya majeneza lililobeba mwili wa aliyekuwa Balozi wa Italia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Luca Attanasio na mlinzi wake, Vittorio Iacovacci baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Ciampino mjini Rome, Italia leo Februari 24, 2021 kwa ajili ya taratibu za maziko ikiwa ni siku chache baada ya kuuawa na watu wasiojulikana nchini DRC. (Picha na Reuters/ Diramakini).

Balozi Attanasio aliuawa katika shambulizi la kuvizia karibu na mji wa Goma Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mlinzi wake, pia raia wa Italia pamoja na dereva wao ambaye ni raia wa Congo nao walipoteza maisha katika shambulizi hilo.

Waziri Di Maio ametoa wito huo leo Februari 24, 2021 amesema ametoa ombi rasmi kwa Shirika la Chakula Duniani (WFP) pamoja na Umoja wa Mataifa kuanzisha uchunguzi ili kubaini kilichotokea.

Amesema , uchunguzi huo utataka kujua namna mipangilio ya kiusalama ilivyoshughulikiwa, hali kadhalika aliyehusika kuchukua maamuzi.

Mwili wa balozi huyo umewasilishwa leo mjini Rome,Italia na kupokelewa uwanjani na Waziri Mkuu Mario Draghi.

Awali Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeelezea kusikitishwa kwake na kutuma salamu za rambirambi kwa familia, wafanyakazi na marafiki wa watu watatu waliouawa katika shambulio dhidi ya ujumbe wa ubalozi wa Italia uliokuwa ukizuru mashinani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Ujumbe huo ulikuwa unasafiri kutoka Goma kuzuru programu ya WFP ya mlo shuleni katika eneo la Rutshuru wakati shambulio hilo lilipotokea.

WFP ilieleza itashirikiana na mamlaka ya DRC kubaini taarifa zaidi za waliohusika na shambulio hilo lililotokea katika barabara ambayo iliruhusiwa watu kusafiri bila kusindikizwa na vikosi vya usalama.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alilaani vikali shambulio hilo dhidi ya msafara wa pamoja wa Shirika la WFP na ubalozi wa Italia huko Kibumba karibu na Goma mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

“Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Italia na DRC huku akielezea mshikamano wake na wafanyakazi wa WFP na timu nzima ya Umoja wa Mataifa nchini humo,”ilieleza taarifa ya msemaji wa Guterres iliyotolewa jiijni New York, Marekani.

Katibu Mkuu alitoa wito kwa serikali ya DRC kuchunguza haraka tukio hilo na washukiwa wafikishwe mbele ya sheria huku akisema kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia serikali na watu wake katika kusaka amani ya kudumu mashariki mwa nchi hiyo.
 
Balozi Attanasio ambaye ana umri wa miaka 43 ameiwakilisha nchi yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu mwaka 2017.

Post a Comment

0 Comments