Mapinduzi ya Kijeshi nchini Myanmar yazua hofu

Kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi na wenzake kutoka chama tawala wamewekwa kizuizini na Jeshi kufuatia ukamataji uliofanywa asubuhi ya Jumatatu kwa saa za huko, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kwa mujibu wa msemaji wa chama cha kitaifa cha Democracy,Myo Nyut hatua hiyo ilikuja baada ya siku kadhaa za kuongezeka mvutano kati ya serikali ya kiraia na jeshi lenye nguvu ambalo lilichochea hofu ya mapinduzi baada ya uchaguzi ambao jeshi linasema ulijaa ulaghai.

Nyut amelieleza shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba, Suu Kyi, Rais Win Myint na viongozi wengine walichukuliwa mapema asubuhi kwa saa za huko.

"Ninataka kuwaambia watu wetu wasijibu kwa haraka na ninawataka wachukue hatua kulingana na sheria,"amesema Msemaji huyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Msemaji wa jeshi hakujibu simu zinazomtaka kutoa maoni yake kuhusiana na suala hili la kuwaweka kizuizini viongozi hao.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelaani vikali kushikiliwa kwa viongozi wa kisiasa na maafisa wa serikali ikiwemo kiongozi mkuu wa Myanmar Aung San Suu Kyi na rais Win Myint na jeshi la nchi hiyo.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu ameelezea wasiwasi mkubwa kufuatia kutangazwa kwa kupinduliwa kwa mamlaka ya bunge, rais na mahakama kwenda kwa jeshi.

Taarifa ya Katibu Mkuu ilimnukuu akisema, “matokeo haya ni pigo kwa mabadiliko ya kidemokrasia nchini Myanmar".

Tukio hilo lilikuja saa chache kabla ya kufunguliwa rasmi kwa kikao kipya cha bunge. Siku chache kabla ya tukio hilo kulikuwa na ongezeko la uhasama kati ya serikali na jeshi baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba.

Aung San Suu Kyi anayeongoza chama cha National League for Democracy (NLD) aliibuka mshindi na kupata asilimia 80 ya viti katika bunge kwa mujibu wa ripoti kutoka vyombo vya habari.

Hata hivyo jeshi na baadhi ya vyama vya kisiasa walipinga matokeo hayo kwa madai kwamba upigaji kura ulikuwa na makosa.

Katibu Mkuu amehimiza viongozi wa kijeshi kuheshimu matakwa ya watu wa Myanmar na kuzingatia demokrasia na kutatua tofauti zozote kwa njia ya majadiliano ya amani.

"Viongozi wote ni lazima wazingatie mabadiliko ya kidemokrasia Myanmar na kushirika majadiliano ya muhimu na kujizuia kutokana na ukatili na kuheshimu haki za binadamu na uhuru,"amesema.

Katibu Mkuu alihakikisha uungwaji mkono watu wa Myanmar katika kutafuta demokrasia, amani, haki za binadamu na kusimami sheria.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, kushikiliwa kwa viongozi hao kulianza Jumatatu nchini Myanmar huku viongozi wa kisiasa wakishikiliwa Yangon na miji mingine Myanmar huku wanajeshi wakiwa mitaani na katika maeneo makubwa nchini.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa, jeshi limetangaza hali ya dharura kwa mwaka mmoja kupitia televisheni inayofadhiliwa na jeshi huku televisheni za taifa na kimataifa zikiwa hazipatikani kwenye mtandao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news