NELICO,UVCCM kupambana na utegemezi wa ajira za serikalini

Shirika lisilo la kiserikali la NELICO na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Geita wameanza kutoa mafunzo maalum kwa vijana ili waweze kujiajiri badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.

Rahel Ndegeleke ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa wa Geita (aliyesimama) akifungua mafunzo ya siku ya ujasiriamali kwa vijana wa CCM mkoa wa Geita, wengine ni Mkurugenzi wa Nelico, Paulina Alex (kushoto) na Richard Jaba,Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Geita (kulia). (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Shirika la Nelico limetoa mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa wilaya zote za mkoa wa Geita wa UVCCM pamoja na maafisa maendeleo ya jamii wilaya zote za mkoa wa Geita ili kuwajengea uwezo wa kubuni na kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi katika maeneo yao ili waweze kujiari wenyewe.

Akizungumza katika semina hiyo ambayo imelenga kuwapa uwezo wa vijana kuwa wajasiriamali Katibu wa CCM Mkoa wa Geita, Rahel Ndegeleke amesema uchumi na siasa vinatoka chumba kimoja hivyo semina ya ujasiriamali kwa vijana hao ni muhimu.

Amesema , ni muhimu vijana kuweza kujitegemea kiuchumi ili waweze kujikwamua na umasikini na utegemezi huku akishukuru NELICO kufadhili mafunzo hayo kwa vijana.

Katibu Rachel Ndegeleke ameomba mafunzo hayo kutumika kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huo hasa kwenye uchimbaji wa madini,kilimo pamoja na ufugaji wa nyuki kwa ajili ya asali.

Amesema kuwa, utafiti umeonyesh kuwa asali inayozalishwa katika Wilaya ya Bukombe na inayozalishwa Tabora ni asali bora hapa nchini,hivyo vijana hao waitumie kama fursa kwao kiuchumi.

Rahel Ndegeleke amemshukuru Mkurugenzi wa NELICO, Paulina Alex kwa kukubali kufadhili mafunzo hayo ya siku mbili kwa vijana hao kwani yatazaa matunda kwa kuongeza maarifa kwa kuibua fursa mbalimbali.

Amesema kuwa, Mkurugenzi huyo wa NELICO amekuwa mwanamke wa kuigwa na wengine kwani ameongoza shirika hilo kwa zaidi ya miaka kumi kwa mafanikio makubwa na limefanya mambo mengi katika jamii ya mkoa wa Geita.

Mkurugenzi wa NELICO, Paulina Alex amesema mafunzo yatawajengea uwezo vijana hao kuibua miradi mbalimbali ya kuwasaidia kujiajiri kutokana na mazingira yanayowazunguka.

Amesema, Malengo ya NELICO ni kutoa mafunzo hayo kwa vijana hadi ngazi ya kata na kijiji na baada ya mafunzo hayo shirika hilo kwa kushirikiana na UVCCM watatoa kazi za kufanya na kufanya tathimini.

Paulina Alex amesema baada ya tathimini hiyo,watapata mwelekeo ili waweze kuwafikia vijana wengi zaidi hadi ngazi ya kata zote za mkoa ili kijana aweze kujiajiri na kuachana na utegemezi kwa kusubiri ajira za serikali.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Geita, Richard Jaba amesema kuwa, waliomba msaada wa ufadhili wa mafunzo hayo kwa vijana wa CCM mkoa huo baada ya kuona vijana wengine wamekuwa na tabia ya kutegemea ajira za kuajiriwa tu.

Amesema kuwa, ajira za serikalini haziwezi kutosha kila mtu hivyo wao kama UVCCM wameona washirikiane na NELICO kuandaa vijana ili wapate ubunifu wa kuwawezesha kuibua fursa za kiuchumi na kuweza kujiajiri.

Amesema kuwa, suala la ujasiriamali nu muhimu kwa kila kijana hivyo anaangalia uwezekano wa kuendelea kushirikiana na NELICO ili mafunzo hayo yawafikie vijana hadi kwenye ngazi za kata.

Mkufunzi wa semina hiyo kutoka Shirika la Himiza, Justice Bernard Otieno amesema kuwa mafunzo yaliyotolewa kwa vijana hao ni pamoja na Uongozi, kujitambua na kuibua fursa na ujasiriamali.

Wakili Benard Otieno ambaye ni Mkurugenzi wa Shirikia la Himiza Justice akiendelea kutoa mafunzo kwa vijana wa CCM mkoa wa Geita. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Amesema, baada ya mafunzo hayo wanategemea kuona UVCCM mkoa wa Geita inakuwa mfano kwa kuibua miradi yenye tija ili kuendana na Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25.

UVCCM kwa ufadhili wa Shirika la NELICO kupitia Mkurugenzi wake, Paulina Alex wameendesha mafunzo kwa vijana wa mkoa mzima kwa kuanzia na viongozi wanne kila wilaya kwa muda wa siku mbili mfululizo, mafunzo ambayo baadae yanalenga kuwafikia vijana hadi ngazi ya kata na vijiji.

Post a Comment

0 Comments