Viongozi wa dini Malawi waitaka Serikali kusitisha kupokea chanjo ya Corona,ikikaidi waumini wataisusia

Wakati mataifa mbalimbali ya Afrika yakitarajia kupokea zaidi ya dozi milioni 90 za chanjo ya virusi vya Corona (Covid-19),baadhi ya mataifa wakiwemo viongozi wa kidini wameanza kutilia mashaka chanjo hizo, anaripoti Mwandishi Diramakini (Lilongwe).

Haya yanajiri baada ya Afrika Kusini kutilia mashaka chanjo mapema wiki hii, ambapo kwa sasa viongozi wa dini nchini Malawi wameitaka Serikali yao na wananchi kutokubali chanjo hizo kwa kuwa zinaonekana si salama.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake kupitia Muungano wa The Freedom of Worship Association of Malawi (FOWAM),Nabii David Mbewe amesema, chanjo ya AsdtraZeneca si salama kwa matumizi, hii ikiwa ni kutokana na tafiti za karibuni.

Amesema, kutokana na mapungufu hayo hawapaswi kuzitumia iwapo zitafika mapema mwezi huu kama ilivyopangwa, badala yake waendelee kumtegemea Mungu na kuzingatia miongozo na kanuni za afya kwa mujibu wa Wizara ya Afya nchini humo.

Nabii David Mbewe ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Living Word Evangelical Church (LIWEC) ambaye pia ni Rais wa Muungano huo akiwa na Msemaji wake, Jerafaya Geoffrey Phomea wameonya kuwa, iwapo mamlaka za juu zitashindwa kutilia maanani wito huo watatoa wito kwa waumini wao kususia kuchanjwa chanjo hiyo.

Amesema, raia wa Malawi hawapaswi kutumika kufanyiwa majaribio ya chanjo ambazo bado hazijaonyesha majibu sahihi.

"Iwapo watafanya uamuzi wa kuruhusu Wamalawi wachanjwe chanjo hiyo watakuwa wameamua kuyaweka maishaya ya raia wasiokuwa na hatia katika hatari kubwa zaidi kiafya, unaweza kuona wazi kuwa tayari ndugu zetu wa Afrika Kusini wamesitisha zoezi la kuchanja raia wao kupitia chanjo hiyo baada ya kubaini mapungufu mengi, hivyo hatupaswi kufanya majaribio kwa rai wetu,"ameeleza kupitia taarifa hiyo.

Wakati huo huo Mpango wa Kimataifa wa Kuratibu chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona (COVID-19) wa COVAX, umesema kuibuka kwa minyumbuliko tofauti ya virusi aina ya SARS-CoV-2 vinavyosababisha COVID-19 ni kumbusho thabiti kuwa virusi hivyo vina uwezo wa kubadilika na hivyo hatua za kisayansi zinapaswa kuendana na mazingira ili ziweze kukabili virusi hivyo.

Mashirika yanayounda mpango wa COVAX yamesema hayo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa katika miji ya Geneva, Uswisi, Oslo Norway na New York, Marekani kufuatia ripoti za hivi majuzi ya kwamba chanjo dhidi ya Corona aina ya AstraZeneca/Oxford ina uwezo mdogo wa kuzuia ugonjwa Corona usababishwao na mnyumbuliko mpya wa virusi B.1.351.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa ni muhimu kutambua kuwa uchambuzi wa msingi kutoka awamu ya tatu ya majaribio ya chanjo hiyo hadi sasa bila kuwepo kwa mnyumbuliko huo mpya wa virusi, ina uwezo wa kinga dhidi ya ugonjwa wa Corona unapokuwa katika hali mbaya zaidi, kama vile mgonjwa akiwa hospitalini au anakaribia kifo.

Kwa mantiki hiyo COVAX inasema ni muhimu sana hivi sasa kubaini uthabiti wa chanjo pindi linapokuja suala la kinga pindi mgonjwa anapokuwa taabani baada ya kuambukizwa aina mpya ya virusi vya Corona.

Taarifa hiyo ilisema uchambuzi zaidi utawezesha pia kuthibitisha ratiba sahihi ya utoaji wa chanjo hiyo na ufanisi wake.

Kwa upande wake watengenezaji wametakiwa kujiandaa juu ya mabadiliko ya virusi aina ya SARS-CoV-2 ikiwemo kutoa chanjo za kuongeza nguvu na ziendanazo na virusi vilivyopo iwapo itaonekana lazima kufanya hivyo,

Mapema akizungumzia minyumbuliko ya virusi, Dkt. Richard Hatchett, ambaye ni Afisa Mtendaji wa Ushirika wa ubunifu wa maandalizi dhidi ya milipuko ya magonjwa, CEPI, alisema, “Unafahamu tulitarajia bila shaka virusi hivyo vinaweza kubadilika. Wanasayansi kwenye maabara walitarajia hivyo na hii ndio moja ya mambo mazuri kwenye sayansi. Inakuwezesha kuangazia siku za usoni na mambo yanayoweza kutokea na kuangazia mabadiliko yanayoweza kuleta madhara.”

Hata hivyo, COVAX imeendelea kusisitiza kuchukuliwa kwa kila hatua kupunguza kusambaa kwa virusi, kuzuia maambukizi yanayoweza kutoa fursa zaidi ya virusi SARS-CoV-2 kunyumbulika na kupunguza ufanisi wa chanjo za sasa.

Hata hivyo Afrika Kusini imesitisha kwa muda kampeni yake ya chanjo dhidi ya virusi vya Corona (COVID-19) baada ya utafiti mpya kubaini kuwa chanjo ya AstraZeneca haifanyi kazi vizuri dhidi ya aina mpya ya virusi vinavyopatikana nchini humo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Utafiti huo, uliofanywa na Chuo Kikuu cha Witwatersrand huko Johannesburg umehitimisha kuwa chanjo ya Uingereza ilitoa tu kinga ndogo dhidi ya aina za wastani za ugonjwa unaosababishwa na aina tofauti ya virusi huko Afrika Kusini kwa vijana.

Haya yanajiri ikiwa tangu awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliwatahadharisha Watanzania na mataifa mengine ya Afrika juu ya matumizi ya chanjo za magonjwa mbalimbali zinazotoka mataifa nje ya Afrika kwa kwa ajili ya kukabili maambukizi ya magonjwa hayo.

Rais Magufuli akiwa katika hafla ya kitaifa iliyofanyika wilayani Chato mkoani Geita hivi karibuni aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Dkt. Magufuli alitoa angalizo kwa watanzania kuacha kukimbilia chanjo dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 na magonjwa mengine sugu.

Rais Magufuli ingawa hakusema moja kwa moja kwamba maambukizi ya ugonjwa wa Corona yapo nchini, alitaka tahadhari ichukuliwe ikiwemo wananchi kujifukiza, kula vizuri na pia kuendelea kumuomba Mungu kwani yeye ndiye muweza wa mambo yote.

Aidha, Rais aliwataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi huku wakichukua tahadhari za kiafya kwa vile hana mpango wa kuzuia watu kutoka nje kwa kusisitiza kuwa taifa la Tanzania halitaweza kujifungia ndani kutokana na changamoto za Corona.

Wakati huo huo, Afrika Kusini ilikuwa imepanga kuanza kuchanja watu wake kwa dozi milioni moja za chanjo ya AstraZeneca katika siku zijazo.

Utafiti uligundua kuwa chanjo hiyo ilikuwa na ufanisi wa asilimia 22 tu katika visa vya wastani vya aina ya ugonjwa huo wa Afrika Kusini.

Hatua hiyo inatajwa kuwa pigo kwa mipango ya awali ambayo ilielezwa kuwa, chanjo milioni 90 za ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) zitaanza kusambazwa barani Afrika mwezi huu katika kile ambacho kinaelezwa kuwa kitakuwa kampeni kubwa zaidi ya chanjo barani Afrika.


Hayo ni kwa mujibu wa mfumo wa kusambaza chanjo za COVID-19, COVAX ulioundwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake.


Chanjo hiyo aina ya AstraZeneca/Oxford AZD1222 iliorodheshwa kwa matumizi ya dharura na WHO ambapo shirika hilo sasa lilikuwa linathamini chanjo hiyo na matokeo yatatangazwa karibuni.

“Afrika imeshuhudia maeneo mengine yakianza utoaji wa chanjo ya COVID-19, yenyewe ikiwa kando. Mpango huu wa kupeleka chanjo ni hatua ya kwanza muhimu katika kuhakiisha kuwa bara hilo linapata fursa sawa ya chanjo kama maeneo mengine,”alisema Dkt.Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika akizungumza katika mkutano na wanahabari kwa njia ya mtandao huku akiongeza kuwa, “tunatambua kuwa hakuna aliye salama hadi pale kila mtu atakuwa salama.”

COVAX kupitia barua yake ya Januari 30, mwaka huu ilijulisha nchi za Afrika kuhusu mpango huo wa upelekaji chanjo.

Kutokana na kiwango kikubwa cha mahitaji ya chanjo ya COVID-19, shehena za mwisho zitategemea kiwango cha uzalishaji kutoka kwa kampuni husika na utayari wa nchi kupokea chanjo hizo.

Nchi zinazopokea chanjo hizo zinatakiwa kuwasilisha mipango yao ya mwisho ya usambazaji na utoaji wa chanjo hiyo kutoka COVAX. (Imeandaliwa na Mwandishi Diramakini ).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news