BREAKING NEWS: Bunge la Tanzania lamthibitisha Dkt.Philip Isidory Mpango kuwa Makamu wa Rais Mteule

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limemthibitisha aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Isidory Mpango na Mbunge wa Buhigwe mkoani Kigoma kuwa Makamu wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).

Akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Machi 30, 2021 bungeni jijini Dodoma, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema,kura zilizopigwa ziliongezeka hadi 363.

"Hakuna kura iliyoharibika hata moja, hivyo naomba kulitangazia Bunge hili na Watanzania kwa ujumla kwamba, kura zote 363 ni kura za ndiyo na kwa hiyo amepata asilimia 100,"amesema Spika Ndugai huku akiongeza kuwa, kwa mujibu wa Katiba anasubiri kuapishwa.

Spika Ndugai amesema kuwa baada ya jina lake kuthibitishwa na Bunge, Katiba inaweka wazi kwamba jimbo la Buhigwe sasa liko wazi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itaendelea na mchakato wa kutangaza rasmi ratiba ya uchaguzi mdogo kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo ambayo imeachwa wazi baada ya Dkt.Mpango jina lake kuthibitishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais.

Spika Ndugai kabla ya kutangaza matokeo alimpa nafasi Dkt.Mpango ya kuzungumza kwa mara mwisho ndani ya Bunge hilo kwani baada ya hapo hataruhusiwa kuzungumza chochote kwa mujibu wa Katiba.

Kabla ya kumkaribisha Dkt.Mpango, Spika Nduga aliwaambia wabunge kwa mujibu wa Katiba jina lake likashapitishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hataweza kuzungumza bungeni, hivyo ni vema akazungumza kabla ya jina kuthibitishwa na Bunge.

"Nimehangaika sana kupata jibu la nini tufanye, nimeangalia katiba yetu inaeleza wazi kabisa, hivyo tukisubiri athibitishwe na Bunge kisha aseme haitawezekana, hivyo azungumze kabla jina halijathibitishwa.Kuna watu huko nje huko wataanza kusema Spika hakufuata Katiba.Dkt.Mpango karibu uzungumze na wabunge kwa mara mwisho humu ndani,"amesema Spika Ndugai.
Kwa upande wake, Dkt,Mpango amesema kuwa, anamshukuru Mungu kwa siku ya leo ambayo imekuwa muhimu kwake.

"Siku ya leo sina maelezo lakini naomba muendelee kunisaidia kushukuru Mungu pamoja nami, kwa miaka mingi nimekuwa kwenye nafasi mbalimbali.Nimekuwa nasumbuka sana na umasikini, kwasababu ile ile nimevaa kiatu cha umasikini toka utoto wangu, ndio maana hata nilipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nisilisoma uchumi wa maedeleo.

Inapofika siku hii ambayo wabunge mtanithibitisha katika nafasi ambayo Rais amependekeza, kazi yangu ya kwanza kumsaidia ni kuhakikisha ndoto ya watanzania inatimia.

"Sote ni mashahidi, nataka kukumbusha matukio mawili, wakati tunaomboleza, wananchi wanyonge kabisa kule Dar es Salaam waliruka fensi kwenda kumsikiza kipenzi chao Hayati Magufuli wakati mwili wake unataka kupakiwa kwenye ndege kuja DodomaTukio la pili nilishuhudia hapa Dodoma bodaboda walivyoamua kumsikindikiza kipenzi chao.

"Matukio haya mawili yanatoa ujumbe kazi ambazo zimeachwa na kipenzi chetu zisipokwenda vizuri hatuna namna, kwa hiyo tunatakiwa kuhakikisha ndoto za watanzania zinatimia, wanataka SGR yao ikamilike, wanataka bwawa la Mwalimu Nyerere likamlike, wanataka barabara na hasa za vijijini zikamilike.

"Wanataka huduma za afya ziwe bora zaidi, wanataka maji safi na salama, wanataka usalama wao waendeee kufanya shughuli zao.Hawataki rushwa, nachotaka kusema kama Bunge litanithibitsha haya ndio mambo nitakayokwenda kumsaidia Rais wetu ili nchi yetu isonge mbele, kiu ya wananchi itimie.Bunge ni chombo muhimu sana na katika miaka mitano na kidogo nimejifunza sana.

"Spika nataka nikushukuru wewe binafsi, mtangulizi wako alikuwa spika wa viwango, nadhan wewe ni Spika wa kidigital, umekuwa kiongozi mahiri, ukifika msimamo ni msimamo, mambo ya msingi lazima tusimamie, umeendesha Bunge hili vizuri licha ya kuwa na pande mbili,"amesema Dkt.Mpango wakati anaaga Bungeni.

Pia amempongeza Naibu Spika Dkt.Tulia Ackson kwa jinsi anavyotekeleza majukumu yake ndani ya Bunge kwani amekuwa mwanamke shupavu na imara wakati wote."Waziri Mkuu una namna nyingi za kukuelezea, wakati wa hotuba sikutarajia kila alipozungumza alikuwa anasema mawaziri wenzangu ahsante kwa unyenyekevu.

"Wabunge hawa wakinipitisha nitajifunza kwako unyenyekevu, najua ulikuwa uhalili ili kumsaidia Rais na Makamu wa Rais katika kufanya kazi ambazo wakubwa wetu walikuwa wanakutuma, umekuwa darasa.Nawashukuru Kamati za Bunge, nimeshuhudia ushirikiano mzuri kati ya Wizara yangu na kamati zote, ahsanteni sana maana hiyo ndio inatupasa.Kazi hizi tufanye kwa uaminifu kabisa.

"Na mimi mkinithibitisha naomba Mungu anisaidie yale ambayo yatashauriwa na Bunge nitamshauri Rais yatekelezwe.Mimi ni binadamu najua kuna mengine hamkusema, kama nilimkwaza mtu yoyote naomba mnisamehe, na mimi sitatoka kabisa na lalamiko lolote juu ya mbunge yeyote.

"Najua mmesema mimi ni mpole, mcha Mungu, najitahidi maana bila yeye mimi si chochote.Muwe mnasema ukweli mimi sio mpole kiasi hicho, kwenye mambo ya hovyo hovyo sio mpole, kwenye mambo ya ubadhirifu wa fedha za umma mimi sio mpele, kwa watu wanaokula rushwa mimi sio mpole.

"Naomba mnisamehe, pale ambapo nitatakiwa kusimamia mambo kwa maslahi ya umma nitamshauri rais twende sawa, umasikini katika nchi yetu ni mkubwa, watu zaidi ya milioni 14 wanaishi chini ya kiwango cha umasikini, hii haiwezekani.Kwa hiyo wale ambao wanadokoa fedha za umma wale ni halali yangu.Naomba Mungu nisiwe na chuki na mtu yoyote wala nisionee yoyote,"amesema Dkt.Mpango.

Dkt.Mpango ametumia nafasi hiyo kutoa ombi kwa wabunge wote kusimama imara katika kupigania maslahi ya Taifa huku akitoa ujumbe kwa wabunge wa upinzani kuhakikisha kwenye maslahi ya nchi wanatoa ushirikiano.

"Niseme ukweli nilikuwa naumia sana ninapowasilisha bajeti kwa ajili ya kusaidia wananchi masikini, wapinzani wanakaataa.Naomba tuwe wamoja, na pale ambapo kuna mambo ya msingi msisite simameni imara kuyasemea,"amesema Dkt.Mpango.

Aliyanena haya Dkt.Mpango baada ya jina lake kutajwa bungeni

"Kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa namna ya pekee kabisa kwa kutupatia uhai na kutuwezesha kukutana hapa ili kuendelea na shughuli zetu za kikatiba.Pili napenda kumshukuru sana mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kupendekeza jina langu na kuridhiwa na chama chetu ili liweze kuletwa hapa. 

"Hii ni nafasi muhimu sana na nyeti ya makamu wa rais ni heshima kubwa sana sikuwahi kuota, wakati naibu wangu anajibu swali nilikuwa nahangaika kwenye mambo mengine ikiwemo mishahara ya baadhi ya wabunge, nimetoka nje mara kadhaa kujaribu kuhangaika, lakini nimepigwa na butwaa,"amesema Dkt.Mpango.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupendekeza jina la Dkt.Mpango kuwa Makamu wa Rais na kuliwasilisha mbele ya Bunge leo Machi 30,2021.

Dkt.Mpango alizaliwa katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma mwaka 1957. Alisoma shule ya msingi Kipalapala na Muyama, alijiunga seminari ya Ujiji na baadaye seminari ya Utaga Tabora. Alijiunga kidato cha tano na sita katika sekondari ya Ihungo, Bukoba na alihitimu mwaka 1977 na kujiunga na jeshi la kujenga Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news