Hope for Girls and Women Tanzania washirikiana na Wilaya ya Serengeti kutoa elimu madhara ya ukatili

NA FRESHA KINASA

Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara wametoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji, kurithi wake na ndoa za utotoni kwa vijiji mbalimbali vilivyopo wilayani humo katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika leo Machi 8.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake ambapo Wilaya ya Serengeti imeyafanyia Kijiji cha Mbalibali. 

Lengo ikiwa ni kuihimiza jamii kuwathamini wanawake na kutowafanyia vitendo vya kikatili vilivyo kinyume na sheria za nchi na haki za binadamu katika kuhakikisha usawa na haki vinaimarishwa kwa ustawi thabiti wa jamii endelevu.

Mkurugenzi wa Shirika la HGWT, Rhobi Samwelly amesema, lengo la kutoa elimu kwa vijiji hivyo ni kutaka jamii ipate uelewa thabiti wa madhara ya ukatili kusudi ishiriki katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo ambayo pia huchangia kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia katika jamii.

Rhobi ameongeza kuwa, katika kuimarisha usawa wa kijinsia katika jamii elimu ni nyanja muhimu kujenga uelewa kwa Wananchi hasa kuwaelimisha madhara ya mila zisizofaa ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake pamoja na vitendo vya manyanyaso ambavyo hudidimiza usawa na kuliacha nyuma kundi la wanawake.
Rhobi Samwelly akiwa na baadhi ya Wasichana waohifadhiwa Kituo Cha Nyumba Salama Mugumu Serengeti kufuatia kukimbia Ukatili katika familia zao.Kituo hicho kipo chini ya Shirika la (HGWT). 

"Tumeshirikiana na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii kuifikishia Jamii elimu ya madhara ya ukatili. Makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, Vijana, Wazee wameweza kuelimishwa kusudi sasa watambue kuwa Mwanamke ni muhimu katika Maendeleo ya Jamii, Taasisi, na hata maendeleo ya Taifa letu na hivyo wathamini usawa na kuondokana na mfumo dume ambao pia hukandamiza haki za Wanawake,"amesema Rhobi.

Naye Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Serengeti, Isack Mwakyusa amesema kuwa, katika zoezi zima la utoaji elimu waligundua wanawake wengi hunyanyaswa na kukaa kimya badala ya kutoa taarifa katika vyombo vya kisheria kwa hatua stahiki.

Aliongeza kuwa, huu ni wakati mwafaka kupaza sauti kupinga ukatili na unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya watu dhidi yao, hatua ambayo itaimarisha usawa na haki katika kufikia malengo ya Serikali ya kumkwamua wanawake na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya jamii na Taifa.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Kamala amesema wanawake wengi wilayani humo hufanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo kupigwa na waume zao, kunyanyaswa, kutelekezwa wakiwa na Watoto wachanga pamoja na kunyimwa fursa ya kumiliki rasilimali mbalimbali na hivyo kuomba msaada kwa Mkuu wa Wilaya ili wanusuru maisha yao.

"Yupo mama mmoja alifika kwa Mkuu wa Wilaya akiwa amefanyiwa ukatili mkubwa sana na mme wake alisema ana watoto watatu na mtoto wake wa mwisho alikiwa na mchanga akaniambia amepigwa na mme wake na amefukuzwa nilichokifanya nikamtafutia nauli ya kwenda kwao, alisema mme wake alikuwa amemtangazia uamzi mgumu. Niliwasiliana na Mtendaji anakoishi nikamwambia amkamate nashukuru yule mama aliitwa kule na Mtendaji nadhani waliyamaliza kwani hajanipigia tena.kifupi ukatili bado upo,"amesema Cosmas.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu aliyekuwa mgeni rasimi katika maadhimisho ya siku ya Wanawake yaliyofanyika katika Kijiji Cha Mbalibali wilayani Serengeti kiwilaya, aliwaomba Wazee wa kimila kuisaidia Serikali kumaliza vitendo vya ukeketaji, ndoa za utotoni, kurithi wake kwani vimepitwa na wakati na vinamadhara kiafya.

Aidha, Babu aliwaomba wananchi wilayani humo kuwathamini watoto wa kike na kutowakatisha masomo ili kuwaozesha kwa lengo la kupata mali, akisisitiza wanawake kujiamini katika masuala mbalimbali hususan kutumia dhamana vyema kwa wale walioaminiwa kuongoza.

Pia, alipiga marufuku tabia ya baadhi ya wazazi kuwazuia Watoto wao kwenda shule ili wakachunge ng'ombe, ambapo alisema yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua Kali za kisheria kwani kufanya hivyo ni kufifisha malengo ya Serikali ya kutoa elimu bure kwa Watoto wote Nchini.

Neema Jackson na Ester Marwa Wakazi wa Kijiji Cha Mbalibali Wilayani Serengeti wakizungumza na DIRAMAKINI kwa nyakati tofauti wamepongeza kazi kubwa zinazofanywa na Shirika la HGWT katika kupigania haki za Wanawake dhidi ya aina mbalimbali za Ukatili Jambo ambalo kwa Sasa limewafanya wananchi kujitokeza kutoa taarifa katika vyombo vya sheria.
Rhobi Samwelly akiwa na Mabinti wa Nyumba Salama Mugumu Serengeti ambao walishiriki maadhimisho ya siku ya Wanawake. Kituo hicho kipo chini ya( HGWT).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news