Tanzania, Uingereza kuandaa Kongamano kubwa la uwekezaji, lengo ni kutangaza fursa zilizopo nchini

Nchi za Tanzania na Uingereza zipo katika maandalizi ya Kongamano kubwa la Uwekezaji litakalohusisha Wawekezaji wan chi hizo mbili lengo likiwa ni kutangaza fursa za Uawekezaji zilizopo nchini Tanzania na kuvutia wawekezaji kutoka nchini Uingereza, anaripoti Grace Semfuko (MAELEZO).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Bw. David Concar wamefanya mazungumzo jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa kongamano hilo litafanyika mwaka huu ambapo sasa mazungumzo ya awali kuhusu kongamano hilo yanaendelea.

Profesa Mkumbo amesema kutokana na Tanzania kuwa na fursa nyingi za uwekezaji huku mazingira ya uwekezaji yakiendelea kuimarishwa, ipo haja kwa wawekezaji wa Uingereza kuja kuangalia fursa na kuwekeza nchini.

"Tumezungumzia fursa za uwekezaji hapa Tanzania, Uingereza inawekeza kwa kiasi kikubwa sana hapa, tumekubaliana Tanzania na Uingereza tunakwenda kuandaa forum kubwa ya uwekezaji ambapo Wawekezaji wa Uingereza watapata nafasi ya kuja kusikiliza fursa za hapa Tanzania, na sisi tutapata nafasi ya kuzungumzia fursa mbalimbali kuhusu kwa nini wawekezaji wa uingereza waje hapa,” amesema.

Amesema, kufuatia nchi ya Uingereza kujindoa kwenye Nchi Wanachama wa jumuiya ya Ulaya, wameona ni muhimu kuelekeza nguvu zao kwenye nchi ambazo zina fursa nyingi za uwekezaji katika kukuza uchumi wa nchi yao na nchi za uwekezaji.

“Tumeona Nchi ya Uingereza imejindoa kwenye Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ulaya, Balozi amejieleza anataka kuweka mkazo Tanzania kwa sababu anaona kuna fursa nyingi, amemwelewa Rais wetu anataka maendeleo, ameona katika kipindi hiki cha miaka mitano jinsi alivyovutia Wawekezaji, na wanaridhishwa na hatua mbalimbali tunazozichukua kama nchi za kuhakikisha mazingira yetu ya biashara na uwekezaji yanakuwa mazuri,”amesema.

Nae Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bw. David Concar amesema, kutokana na uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji yanayofanywa na Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, kuna umuhimu mkubwa wa Waingereza kuwekeza Tanzania.

"Tumeona kuna fursa nyingi za uwekezaji, kongamano litakalofanyika litasaidia Tanzania kujitangaza kwa Wawekezaji wa Uingereza, mara nyingi nawaambia njooni muwekeze huku, kuna mazingira mazuri sana,” amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news