Watumishi wanawake ni wachapakazi mahiri katika Utumishi wa Umma-Dkt.Michael

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael amesema Watumishi wa Umma wanawake ni wachapakazi mahiri katika Utumishi wa Umma nchini, anaripoti James K.Mwanamyoto (OR-utumishi) Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Umma wanawake wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa katika maandamano ya Siku ya Wanawake kimkoa Machi 8, 2021 jijini Dodoma.

Dkt. Michael amepongeza uchapakazi wa watumishi wanawake mapema leo wakati akitoa ujumbe maalum wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani Machi 8, 2021 ikiwa ni sehemu ya ofisi yake kutambua mchango wa Watumishi wa Umma wanawake katika utoaji huduma kwa wananchi.

Dkt. Michael amesema, kutokana na uchapakazi wa watumishi wanawake, Ofisi ya Rais-UTUMISHI iliona kuwa ina wajibu wa kuhakikisha watumishi wanawake wanashirikishwa kikamilifu kwenye nafasi za uongozi.
Afisa Habari wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Veronica Mwafisi akifanya mahojiano na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2021.

Amefafanua kuwa, kwa upande wa nafasi za Ukurugenzi ambapo ofisi ina jumla ya Wakurugenzi 13, wanawake wapo 6 sawa na asilimia arobaini na sita (46%) wakati wanaume wapo 7 ambao ni asilimia hamsini na nne (54%).

Ameongeza kuwa, kwa upande wa Wakurugenzi Wasaidizi ofisi ina jumla ya Wakurugenzi Wasaidizi 22, kati ya hao 12 ni wanawake ambao ni sawa na asilimia hamsini na tano (55%) wakati 10 ni wanaume ambao ni sawa na asilimia arobaini na tano (45%).

“Ukitazama takwimu ya idadi ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi waliopo katika Ofisi yetu inadhihirisha kuwa, Ofisi imetoa fursa za uongozi kwa wanawake ambao pasipo na shaka yoyote wameuthibitishia umma kuwa, wana uwezo kiutendaji kwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu”, amefafanua Dkt. Michael.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akitoa ujumbe kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2021, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa Watumishi wa Umma wanawake katika kutoa huduma kwa wananchi.

Dkt. Michael ametoa wito kwa waajiri katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanawashirikisha watumishi wanawake katika masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya taasisi zao kwani wanao uwezo kiutendaji katika kuhakikisha taifa linapata maendeleo.

Aidha, ametoa wito kwa Watumishi wa Umma katika Taasisi zote za Umma kuwapa ushirikiano wa dhati viongozi wanawake walioteuliwa na mamlaka mbalimbali ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Sanjali na hilo, amewataka Watendaji Wakuu katika Taasisi za Umma kuwapendekeza wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi ili kutoa fursa kwa wanawake kushiriki katika ujenzi wa taifa.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama msimamizi wa masuala ya kiutumishi na utawala bora nchini inaungana na Watanzania na wadau wote Kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2021, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa viongozi wanawake katika Utumishi wa Umma kama kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inavyojianisha kuwa “Wanawake katika Uongozi: Chachu kufikia Dunia yenye Usawa”.
Baadhi ya Watumishi wa Umma wanawake wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kimkoa Machi 8, 2021 jijini Dodoma.

Post a Comment

0 Comments