Waziri Mhagama atatua kero zilizokuwa zikiwasumbua wafanyakazi Shamba la Mkonge la Kigombe Estate

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ametatua kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili wafanyakazi wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate, Wilayani Muheza dhidi ya mwajiri wao kufuatia malalamiko ambayo yaliwasilishwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Muheza).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Wafanyakazi wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited alipokuwa akitatua migogoro ya wafanyakazi hao dhidi ya mwajiri wao.

Akizungumza wakati wa ziara yake hiyo ya kikazi ambayo ilikuwa imelenga utekelezaji wa Maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyoyatoa tarehe 21 Januari, 2021 alipotembelea shamba hilo la Mkonge lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited.

Mara baada ya kusikiliza pande zote mbili Waziri Mhagama alieleza kuwa kutokana na malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa na wafanyakazi inadhihirisha kuwepo na mapungufu makubwa katika utekelezaji wa sheria za kazi ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa migogoro kutokea.
Sehemu ya Wafanyakazi wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited wakisikiliza maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani).

“Mwajiri anawajibu wa kusikiliza kero na malalamiko ya wafanyakazi waliyonayo na kutafuta ufumbuzi kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi wake, mkifanya hivyo mtaongeza tija na ufanisi katika utendaji wa majukumu yenu,” alisema Wazir Mhagama.

Alieleza kuwa, wajibu wa mwajiri ni kufuata sheria na miongozo ya ajira mahala pa kazi ili kila mfanyakazi aweze kupata haki na utekelezaji wa masuala hayo utawawezesha kuwa na mahusiano mazuri kati ya mwajiri na watumishi alionao.
Mbunge wa Jimbo la Muheza Mhe. Hamis Mwinjuma akieleza jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akitatua migogoro ya wafanyakazi hao dhidi ya mwajiri wao.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia wanyonge na imekuwa ikiwasikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Kwetu sisi Mawaziri tumekuwa tukitekeleza hayo kwa kukutana na wananchi mbalimbali ikiwemo mimi Waziri ambaye nasimamia masuala ya kazi nipo hapa kwa ajili ya kutatua kero zenu na kutafuta ufumbuzi wa pamoja ili kujenga mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu yetu mahala pa kazi,” alieleza.
Mmoja wa Wafanyakazi wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited Bi. Rose Niko (aliyesimama kulia) akiwasilisha kero kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akitatua migogoro ya wafanyakazi hao dhidi ya mwajiri wao.

Sambamba na hayo, Waziri Mhagama alitoa maagizo ikiwemo kukitaka Chama cha Wafanyakazi wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited kujenga tabia ya kukutana na mwajiri mara kwa mara kwa kuzingatia tija na uzalishaji wa kiwanda hicho na kushauriana namna ya kuongeza mishahara na posho kwa wafanyakazi wake.

Suala la pili, Maafisa Kazi kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi katika Shamba la Mkonge la Kigombe Estate lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited, wilayani Muheza.

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kusimamia michango ya wafanyakazi hao katika mfuko huo wa hifadhi ya jamii na kuendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi kuhusu fao la upotevu wa ajira ili watambue sheria inawajibika pale mhusika ameachishwa kazi na siyo kuacha kwa hiyari.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kutoka kulia) akijadiliana jambo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bi. Junica Omari (wa tatu kutoka kushoto) (kushoto) ni Mbunge wa Jimbo la Muheza Mhe. Hamis Mwinjuma. (Picha zote na OWM).

Pia alitoa maagizo kwa Mamlaka ya Maji Safi kuhakikisha maji kupima maji yanayotumiwa na wafanyakazi hao ili waweze kupata maji safi na salama. Pia amewataka TRA pamoja na NIDA kushughulika kwa karibu suala la vitambulisho vya uraia ili TRA waweze kuwapatia TIN namba wafanyakazi ambao walisimamishwa kazi kurejea sehemu zao za kazi katika shamba hilo.

Sambamba na hayo Waziri Mhagama alimpongeza Mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa karibu na wafanyakazi hao pamoja na kushirikiana na viongozi wa serikali katika kutatua kero zinazowakabili wafanyakazi hao wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate, lililopo Wilayani Muheza.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Muheza Mhe. Hamis Mwinjuma alieleza kuwa ziara hiyo ya Waziri itarejesha matumaini kwa wafanyakazi hao wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate kutokana na wataalam mbalimbali alioambatana nao hivyo malalamiko na kero mbalimbali za wafanyakazi hao zitapatiwa ufumbuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news