BARABARA YA ITONI-LUSITU KILOMITA 50 KUJENGWA KIWANGO CHA LAMI

Serikali imesema kuwa itajenga Barabara ya Itoni- Lusitu (Km 50) kwa kiwango cha lami hivi karibuni, ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika Mkoa wa Njombe na mikoa jirani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, wakati akizungumza na wananchi wa Luponde mkoani humo, ambao walizuia msafara wake kushinikiza kujengwa kwa barabara hiyo ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (mwenye shati la Batiki), akisisitiza jambo kwa Mhandisi Mshauri, Moon Dong Ryeol (Wakwanza kushoto), anayesimamia barabara ya Itoni- Ludewa- Manda sehemu ya Lusitu- Mawengi (Km 50), alipofika katika mradi huo kukagua maendeleo yake, mkoani Njombe.

“Naomba wananchi wa hapa muondoe hofu, kwani barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami na kwamba ifikapo mwezi wa Tano mwaka huu, Serikali itatangaza zabuni ya barabara hii”, amesema Chamuriho.

Aidha, Waziri Chamuriho amefafanua kuwa Barabara hiyo ni muhimu kwani kukamilika kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kutaboresha uchumi katika mkoa huo na mikoa jirani.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Njombe, Mhandisi, Ruth Shalua (Wapili kushoto), wakati Waziri huyo alipofika mkoani humo kukagua Barabara ya Itoni – Ludewa- Manda (Km 211.4)
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Njombe, Mhandisi, Ruth Shalua, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (mwenye shati la Batiki), alipofika mkoani humo kukagua maendeleo ya mradi wa Barabara ya Itoni – Ludewa- Manda (Km 211.4).

“Barabara hii ni ya kiuchumi, hivyo lazima ijengwe kwa kiwango cha lami, ili kurahisisha huduma za usafirishaji katika maeneo haya ambapo wengi wenu mnalima mazao kama chai, mbao, viazi na mahindi”, amesisitiza Chamuriho.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya Lusitu- Mawengi (Km 50) kwa kiwango cha zege, Waziri Chamuriho amebainisha kuwa barabara hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu, na kumtaka Mkandarasi anayejenga barabara hiyo kukamilisha ujenzi wake kwa wakati.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (Kulia), akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi, Marwa Rubirya (Katikati) pamoja na Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani humo, Mhandisi, Ruth Shalua (Kushoto) kuhusu maendeleo ya mradi wa Barabara ya Itoni – Ludewa- Manda (Km 211.4).

Kwa upande wake, Mbunge wa Njombe Mjini, Mheshimiwa, Deo Mwanyika, ameishukuru Serikali kwa kuona kilio cha wananchi wake, ambao wamekuwa wakiomba kwa muda mrefu kuwekewa lami katika barabara hiyo ya Itoni- Lusitu (Km 50)

Ameongeza kuwa, Barabara hiyo ikikamilika itafungua zaidi fursa za kibiashara katika mkoa huo na mikoa jirani na hivyo kukuza uchumi katika mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Njombe, Mhandisi, Ruth Shalua, amesema kuwa mradi wa barabara ya Lusitu- Mawengi (Km 50), umefika asilimia 68 ambapo kazi zinazofanyika sasa ni ujenzi wa mitaro ya maji na ukataji mkubwa wa milima eneo la Jongojongo na Gangitoroli.
Muonekano wa Barabara ya Lusitu – Mawengi (Km 50) ambayo inajengwa kwa kiwango cha Zege kwa gharama ya Shilingi Bilioni 159. Barabara hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu.
Muonekano wa Barbara ya Itoni – Lusitu (Km 50) ambayo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami hivi karibuni. (PICHA NA WUU).

Ameongeza kuwa mradi huu unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100, kwa gharama ya shilingi Bilioni 159 na kutekelezwa na Mkandarasi M/s Cheonkwang Engineering & Construction Co. Ltd kutoka Korea Kusini.

Barabara ya Itoni- Ludewa- Manda (Km 211.42) sehemu ya Lusitu – Mawengi (Km 50), ilianza kujengwa mwaka 2016 na inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news