Jeshi lawatimua vijana 854 kwa kuanzisha mgomo, kuandamana kwenda Ikulu kushinikiza ajira

Zaidi ya vijana 854 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokiuka taratibu kwa kuanzisha mgomo na kuandamana kwenda Ikulu wakishinikiza kuajiriwa jeshini wamesitishiwa mikataba yao na kurudishwa nyumbani, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo ameyabainisha hayo Aprili 17, mwaka huu katika hafla ya kuwatunuku kamisheni maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jijini Dodoma.

"Aprili 8, mwaka 2021 vijana wetu wa JKT wapatao 854 walianzisha mgomo, kukataa kufanya kazi maeneo mengine na kufanya maandamano kwenda Ikulu kwa madai ya kutaka kumuona Rais ili wadai kuandikishwa jeshini kama walivyoahidiwa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli.

"Vijana hao ni kati ya vijana 2,400 walioahidiwa kuandikishwa jeshini na walifanya uamuzi huo baada ya jeshi kuamua kuwapunguza katika kazi ya ujenzi wa Ikulu Chamwino baada ya kazi kupungua ili waende kufanya kazi katika maeneo mengine lakini wao wakapinga kwa madai wangekosa kuandikishwa jeshini, " amesema Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo

Amebainisha kuwa, jeshi halikuwa na lengo hilo na limelazimika kusitisha mikataba yao kwa kuwa kosa walilolifanya ni sawa na uasi na hauvumiliki kwa namna yoyote ile. LIVE VIDEO
Pia ameeleza kuwa, pamoja na kufanya uchunguzi wa kwa nini walifanya hivyo, jeshi limeamua kutafakari upya mpango wa kuchukua vijana wa kujitolea kwa ajili ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa.

"Kimsingi Jeshi la Kujenga Taifa, si sehemu ya ajira, bali ni sehemu ya kujifunza stadi za kazi, tunasikitika vijana wale walifanya kazi kubwa na walikaa Jeshi la Kujenga Taifa takribani miaka mitatu, kutokana na tukio hili, tunatafakari utaratibu mpya wa vijana wa kujitolea kwenda Jeshi la Kujenga Taifa,"amesema.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo amewataka maafisa hao wapya kuheshimu, kuzingatia, kuthamini na kutunza viapo vyao katika maisha yao yote kwani hivyo ndiyo vinaunda sheria ya ulinzi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news