Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kwamba kwa ujumla Zanzibar haikabiliwi na misuguano ya kijamii kama inayozikumba nchi nyingine kwa kuwa wananchi wa visiwa hivi ni wamoja na hawagawiki kwa misingi ya kikabila, kidini wala kieneo, isipokuwa imekuwa ikikumbwa na mitafaruku ya kisiasa kutokana na viongozi wa kisiasa kuitumia hali hiyo kwa manufaa yao.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Aprili 9, 2021 alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ujumbe huo, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Ndugu Mathew Mwaimu, ulifika Migombani, ofisini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha rasmi kwake pamoja na kuomba ushirikiano katika majukumu yao.
Mheshimiwa Othman aliuambia ujumbe huo kuwa Zanzibar ipo kwenye maridhiano na inadhamiria kuyaendeleza ili isirejee kwenye mazingira yale yale ambayo yalitoa fursa ya kuvunjwa kwa haki za binadamu na kupotea kwa amani.
“Mara nyingi wanasikika watu wakizungumzia kuhusu maridhiano. Lakini ukweli ni kuwa Wazanzibari hawajawahi kuhasimiana. Bali ni tofauti zinazotengenezwa na viongozi kwa maslahi yao binafsi,” amesisitiza Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Pia Ndugu Mwaimu alitumia fursa hiyo kumpa pole Mheshimiwa Othman kwa kifo cha Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
"Kwa hakika tumefiliwa. Maalim Seif alikuwa mtu sahihi sana na siku zote alitanguliza amani mbele. Maalim Seif amekuwa mdau mkubwa wa amani Zanzibar,”amesema Mwenyekiti Mwaimu.
Makamu wa Kwanza ameahidi kwamba ofisi yake itatoa ushirikiano kwa Tume hiyo kila itakapohitajika kufanya hivyo, kwani lengo lake la dhati ni kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo katika nyanja zote, likiwemo eneo la haki za binadamu.
