MTAMBO WA KUTENGENEZA SILAHA WANASWA KANDA YA ZIWA, AK.47 NA RISASI 128

Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kukamata Mtambo maalum uliokuwa unatumika na wahalifu kutengeneza silaha za haramu ili kutenda uhalifu katika maeneo mbalimbali nchini, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Kanda ya Ziwa.
SACP Mihayo Msikhela akionyesha mtambo uliokamatwa na Polisi mkoani Tabora ambao ulikuwa unatumika kutengeneza silaha haramu za kienyeji.(Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Akizungumza na vyombo vya habari Mkuu wa Operesheni Maalum wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Mihayo Msikhela amesema mtambo huo umekatwa katika mkoa wa Tabora.SACP Mihayo Msikhela akionyesha shehena ya Bangi iliyokamatwa katika mkoa wa Kipolisi wa  Tarime-Rorya (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

SACP Mihayo Msikhela amesama hayo wakati akitoa taarifa ya matokeo ya Operesheni iliyofanyika katika mikoa minane ya Kanda ya ziwa ikijumuisha Geita,Kagera,Shunyanga,Tabora,Mwanza,Simiyu,Mara pamoja na mkoa wa Kipolisi wa Tarime Rorya.

Amesema kuwa, operesheni hiyo ilianza mwezi Februari 27, mwaka na kuhitimishwa Aprili 27, mwaka huu na watuhumiwa waliokamatwa ni kutokana na unyang'anyi wa kutumia silaha,mauaji,kuvunja nyumba,wizi wa mifugo ,wizi wa pikipiki na dawa za kulevya.

SACP Mihayo Msikhela akionyesha vifaa vinavyo tumiwa na waganga wa kienyeji kupiga ramli chonganishi (picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amesema, katika zoezi hilo, polisi pia imekamata silaha ya kivita ijulikanayo kama AK.47 iliyofutwa namba za usajili yenye risasi zake 128.

Silaha nyingine zilizokamatwa ni pamoja na Pistol za kienyeji 10 na moja aina ya Glock 17, Shortgun 3, na Bunduki aina ya Gobore jumla zikiwa 37.

Vitu vingine vilivyokamatwa ni pamoja na Bangi kilogramu 3,000 ,Mirungi kilogramu 15,Ekari 15 za Bangi ziliteketezwa katika mikoa ya Mara , Shinyanga na Tarime-Rorya.

Silaha zilizokamatwa kupitia operesheni hiyo. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Vingine ni Pikipiki 52,Gongo lita 1,600, mitambo ya kutengeneza gongo 20,mifugo 43 ambayo ilirudishwa kwa wamiliki wake,vifaa vya kupigia ramli chonganishi, vifaa vya nyumbani kama redio na TV pamoja na vipodozi.

Msikhela ametaja watuhumiwa waliokamatwa kuwa jumla yao ni 728. Watuhumiwa 647 kesi zao zilifika Polisi, 354 walifikishwa Mahakamani, 193 walipelekwa idara nyingine Kama vile uhamiaji,181 waliwekwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi baada ya ushahidi kutokuwa wa kutosha na watuhumiwa 122 kesi zao ziliisha Mahakamani kwa mafanikio.

Mihayo Msikhela amewataka wananchi kuendelea kufichua vitendo vya uhalifu vinavyo fanyika katika maeneo yao huku wakizingatia kutoa taarifa zilizoa sahihi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news