RC Malima awataja wafanyabiashara watano wanaotuhumiwa kufadhili na kuhamasisha kundi la vijana kuingia na kuiba mawe yenye dhahabu North Mara

Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima amewataka wafanyabiashara watano wanaotuhumiwa kufadhili na kuhamasisha kundi la vijana kuingia na kuiba maweye yenye dhahabu ndani ya Mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime kujisalimisha mara moja katika ofisi za makamanda wa polisi Mkoa wa Mara au kanda maalum ya Tarime/Rorya, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Mara).
Malima amewataja wafanyabiashara hao kuwa ni pamoja Rafael Matiku Zakaria mkazi wa Bweri Musoma,Makenge Chacha Nyaisa Mkazi wa Nyamwaga Tarime, Keraha Yohana Chona makzi wa Nyamongo Tarime,Manase Kazota Philemon mkazi wa Buswelu Mwanza na Nyagwisi Charles Marwa mkazi wa Tarime.

Amesema kuwa wafanyabiashara hao kwa pamoja wanatuhumiwa kuhamasisha na kufadhili baadhi ya vijana kuingia kwenye mgodi huo unaomilikiwa kwa ubia kati ya kampuni ya Barrick pamoja na serikali ambapo vijana hao wamekuwa wakiiba mawe hayo yenye dhahabu na kuwapelekea wafanyabiashara hao.

Amesema kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kwamba wafanyabiashara wa madini wanapaswa kufuata sheria na taratibu zinazongoza biashara hiyo huku akisema kuwa sekta ya mdini ikitumika vema ina mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Mkoa,Taifa na mtu mmoja mmoja.

Amesema kuwa kutokana na uchunguzi ambao bado unaendelea wamebaini kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwatumia baadhi ya vijana kufanikisha malengo yao na kusema kuwa serikali haiwezi kufumbia macho vitendo vya aina hiyo na kuahidi kuwa yeyote atakayebainika kuhusika katika suala hilo atachukukiwa hatua za kisheria bila kujali cheo wala uwezo wake wa kifedha.

Malima pia amefafanua kuhusu taarifa za kufukiwa na kifusi ndani ya mgodi huo vijana saba mwezi Desemba mwaka jana ambapo amesema kuwa baada ya kuwepo kwa taarifa hizo vyombo vya ulinzi na usalama vilianza kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli.

Amesema kuwa hata hivyo hakuna mtu aliyepatikana akiwa amefukiwa na kifusi kama ambavyodaiwa badala yake walibaini kuwepo kwa vitendo vya wizi wa mawe ya dhahabu ndani ya mgodi unaofanywa chini ya ufadhili wa wafanyabiashara hao.

Amewataka wanasiasa kuacha kutoa taarifa za uzushi na upotishaji badala yake washirikiane na serikali katika kutokomeza vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma juhudi za serikali za kuleta maendeleo enedelevu kwa manufaa ya wananchi wote kwa kutumia rasilimali zilizopo.

"Tulitakiwa kujiuliza imekuwaje watu ambao sio wafanyakazi wa mgodi huu kudaiwa kufukiwa na kifusi mgodini badala ya kuanza kutoa maelekezo na vitisho kwa serikali maana haiwezekani mtu kuingia ndani na kufukiwa halafu uanze kuilaumu serikali lakini hata hivyo hakuna mtu aliyepatikana akiwa hai au amefariki huko shimoni ila timebaini kuwa kuna wizi unafanyika,"amesema Malima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news