Serikali yajizatiti kudhibiti magonjwa ya nguruwe nchini

Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mlipuko wa magonjwa ya Nguruwe hayajitokezi mara kwa mara nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega leo Aprili 23, 2021 wakati akijibu swali Bungeni lililoulizwa na Mbunge wa Jiombo la Ndanda, Cecil Mwambe.
Ulega amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mikakati kuhakikisha inadhibiti mlipuko wa magonjwa ya nguruwe. Mikakati hiyo ni pamoja na Kuhimiza wafugaji kuacha kufuga nguruwe kwa njia huria, Kuzuia wageni kuingia kwenye mabanda ya nguruwe, Kuhimiza wafugaji kupulizia dawa za kuua virusi na kupe kwenye mabanda na kuweka dawa ya kuchovya kwenye milango ya mabanda, Kuweka katazo la kusafirisha nguruwe na mazao yake kutoka sehemu zenye ugonjwa.

Vilevile Kuhimiza wafugaji kutokuruhusu wachinjaji au wafanyabiashara kuingia katika mabanda na kuchagua nguruwe wa kununua, Wafugaji kuepuka kulisha nguruwe mabaki ya vyakula kutoka kwenye hoteli na migahawa, Kuacha kuchanganya nguruwe wageni na wenyeji kwenye banda moja na Wafugaji kutoa taarifa za ugonjwa au vifo vya nguruwe pindi vinapojitokeza kwa Mtaalamu wa Mifugo aliye karibu.

Mkakati wa Serikali kupitia Wizara ni kuendelea kutoa elimu ya udhibiti kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani, wakiwemo wafanyabiashara na wasafirishaji wa nguruwe pamoja na watoa huduma za Afya ya Mifugo. Kazi hii itaendelea kufanyaka kwa kuzingatia uhalisia katika kila eneo kwa wafugaji wakubwa na wadogo.

Aidha, Ulega amesema suala la motisha kwa wafugaji wa nguruwe serikali itakwenda kuliangalia kuona namna ya utekelezaji wake ili ukuaji wa tasnia ya nguruwe uende sambamba na ukuaji wa mifugo mingine.

Pia amesema kuwa serikali imejipanga vyema kuhakikisha inajenga majosho katika vijiji lengo ni kuhakikisha maeneo ambayo kuna wafugaji kuna kuwa na josho. Mkakati wa serikali ni kuendelea na zoezi la uogeshaji kwani katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mafanikio makubwa ya udhibiti wa magonjwa yaenezwayo na kupe.

Hivi karibuni kulijitokeza mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Nguruwe katika mikoa kadhaa nchini na kusababisha hasara kwa wafugaji. Ugonjwa huu unaosababishwa na virusi, hauna chanjo wala tiba. Njia pekee za kudhibiti ugonjwa wa Homa ya Nguruwe ni kuzingatia kanuni bora za ufugaji wa nguruwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news