Serikali yatangaza mchakato wa kuanza mnada wa chai nchini

Naibu Waziri Kilimo Mhe. Hussein Bashe amekutana na Wadau wa Sekta ndogo ya zao la chai kutoka Serikalini na Sekta binafsi ili kupata mrejesho wa hatua za uanzishwaji wa mnada wa zao la chai nchini na kusisitiza ulazima wa kuanza kwa mnada huo na manufaa yake kwa Wakulima na Taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri Bashe amesema, lengo la mkutano huo ni kujadiliana namna ya kuongeza uharaka wa juhudi za uanzishwaji wa mnada wa chai ambao utaenda sambamba na uanzishwaji wa maabara pamoja na maghala ya kuhifadhi chai hiyo pamoja na ujenzi wa mazingira mazuri ya biashara ya majani ya chai.
Naibu Waziri Kilimo Mhe. Hussein Bashe akiongoza kikao kazi cha Wadau wa Sekta ndogo ya zao la chai Jijini Dodoma leo April 15,2021 pembeni yake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) Dkt. Emmanuel Simbua.Kikao hicho kimewakutanisha Wadau kutoka Serikalini akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai, Nicholous Mahuya, Mkurugeni Mkuu wa Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai, Theophord Ndunguru, Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa za Mazao ya Kilimo (TMX), Godfrey Malekano.

Wadau wengine wa Sekta Binafsi ni pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Angelina Ngalula, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) Dkt. Emmanuel Simbua, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya AGRI – CONNECT, Colin Scott na Wadau wengine kutoka Taasisi zinazotoa huduma usafirishaji wa mizigo katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Angelina Ngalula akichangia jambo katika mkutano huo.Naibu Waziri Bashe amesema, Serikali inafanya juhudi kubwa kuanzisha mnada wa chai nchini, ambapo haukuwepo kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi kwenye Sekta ndogo ya chai ambao utakuwa na manufaa na faida nyingi kwa Wakulima wa chai nchini.

Naibu Waziri Bashe ametoa mfano kuwa usafirishaji wa kontena moja la majani ya chai la urefu wa futi ishirini kutoka Mufindi kwenda kwenye mnada wa Mombasa nchini Kenya; Gharama yake ni shilingi milioni sita (6,000,000) wakati kontena hilo hilo, linasafirishwa kutoka Mufindi kwenda Jijini, Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi milioni tatu (3,000,000).

“Tukipunguza gharama za biashara moja kwa moja na bei kwa Mkulima nayo itapanda. Faida ya pili ya kuwa na mnada nchini ni kuwa tutakuwa na uwezo wa kutawala (Control) bei ya chai sokoni na kuongeza uwazi wa mnyumbuliko wa gharama za uzalishaji wa chai kwa Wakulima wetu.”
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Angelina Ngalula akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) Dkt. Emmanuel Simbua wakifuatilia mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai, Nicolaus Mahuya akichangia mada katika mkutano huo.

“Tatu, tutakuwa na uhakika wa ubora wa madaraja ya chai kwenye soko kwa sababu tutakuwa na maabara yetu; Sasa hivi hatuna uwezo huo kwa kuwa udhibiti wa madaraja ya chai yetu, unafanywa na Waendeshaji wa minada kwenye nchini nyingine”. Amekaririwa Naibu Waziri Bashe.

Naibu Waziri Bashe ameongeza kuwa kwa muda mrefu chai ya Tanzania imekuwa bora na kusisitiza kuwa uanzishwaji wa maabara ya chai hapa nchini, utaongeza ubora wa chai mara dufu kwa kuwa itakuwa rahisi kuitambua chai kwa ubora wake kijiografia.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Angelina Ngalula amesema Sekta Binafsi imejiandaa na itashirikiana na Serikali katika kujenga mazingira mazuri mazuri ya ufanyaji biashara ya majani ya chai na kuongeza kuwa TPSF ipo tayari kununua vifaa vya maabara ya kisasa ya zao la chai pamoja na ujenzi wa majengo maalum kwa ajili ya maabara hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news