Serikali yawahesabia saa Wakurugenzi wa Longido, Same, Uvinza na Bumbuli

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Longido, Same, Uvinza na Bumbuli kujitathmini kama wanatosha kuendelea kuwa katika nafasi hizo.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya Ukusanyaji wa Mapato ya ndani ya Halmashauri katika kipindi cha Julai,2020 hadi Machi,2021 mapema leo Jijini Dodoma.

Amesema, Wakurugenzi wa Halmashauri zilizokusanya mapato chini ya asilimia 75 wanatakiwa kujitathmini na hawa wa Halmashauri 4 wanatakiwa kujitathimini zaidi endapo wanatosha kuendelea kuziongoza halmashauri hizo.

"Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido kwa mara ya pili sasa anaingiza fedha ambazo si za mapato ya ndani kwenye mfumo wamapato ili ionekane wamekusanya zaidi.

"Mara ya kwanza tungeweza kuvumilia lakini kwa mara ya pili sasa ameingiza fedha walizolipwa Fidia kutoa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwenye mfumo wa mapato takribani shilingi Milioni 700, hili hatuwezi kulivumilia tutachukua hatua,"amesema Mhe.Ummy.

Ameongeza kuwa, Wakurugenzi wa Halmashauri za Same, Bumbuli na Uvinza wanapaswa kujithathimini kwa Halmashauri zao kuchangia asilimia 4 tu ya Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2020/21.

"Wakurugenzi wa Halmashauri hizi hawafanyi vizuri kabisa mfano Same wamekusanya shilingi mil. 594 ila wametoa shilingi mil. 26 tu kwa ajili ya maendeleo sasa mil. 26 zinafanya kazi gani ya kueleweka,"alihoji Mhe.Ummy.

Aidha, Mhe. Ummy aliendelea kutaja Halmashauri ya Uvinza kuwa imekusanya shilingi mil. 624 na kwenye maendeleo wamepeleka shilingi mil. 26 tu huku bumbuli Ikikusanya shilingi mil. 336 na kupeleka shilingi Mil.13 tu kwenye miradi ya maendeleo.

Taarifa ya mapato iliyotolewa na Mhe.Ummy inaainisha ufanisi wa kila Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kulinganisha makisio idhinishwa na mapato halisi.

Kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 Halmashauri zilipanga kukudanya Shilingi Bil 814.9 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na katika kipindi cha Julai,2020 hadi Machi,2021 Halmashauri zimekusanya jumla ya shilingi Bilioni 557.45 ambayo ni sawa na asilimia 68 ya makisio ya mwaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news