Waajiri watakiwa kuzingatia maslahi ya watumishi wa umma

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka waajiri katika Taasisi za Umma kutoa kipaumbele kwenye masilahi ya watumishi, ikiwa ni pamoja kuwaasa Maafisa Utumishi kufanya ufuatiliaji ili kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata stahili zao kwa wakati, anaripoti Veronica Mwafisi-Mtwara.

Mheshimiwa Ndejembi ametoa wito huo kwa Waajiri na Maafisa Utumishi akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Manispaa hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na Viongozi walio katika mkoa huo.

Akitoa mfano wa uzembe wa Afisa Utumishi mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mhe. Ndejembi amesema afisa huyo amesababisha watumishi wapatao 236 kutopata stahili ya kupandishwa madaraja kwa kisingizio cha kuchoka jambo ambalo halikubaliki katika Utumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa, kitendo cha kutowapandisha madaraja watumishi hao kwa wakati kimewanyima haki yao ya msingi kwani katika Utumishi watalazimika kutengewa upya bajeti katika mwaka wa fedha mwingine ili waweze kupandishwa madaraja kwa mujibu wa sifa za miundo ya kada zao, ikiwa ni pamoja na kuzingatia uadilifu na utendaji kazi wao.
Baadhi ya Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na Viongozi hao waliopo mkoani humo.

Sanjari na hilo, ameelezea kitendo cha waliokuwa Watumishi wa Umma katika Halimashuri ya Wilaya ya Kibaha ambao mpaka wanastaafu mwaka jana hawakupandishwa madaraja kwa wakati jambo ambalo limeathiri mafao yao.

Kutokana na changamoto ya watumishi hao kutopata stahili, Mhe. Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitomvumilia mwajiri au Afisa Utumishi yeyote atakayesababisha Watumishi wa Umma kutopata masilahi au stahili zao kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.

“Tukibaini kuna Mwajiri au Afisa Utumishi yeyote anayezembea na kusababisha watumishi waliopo kwenye taasisi yake kukosa stahili zao kwa wakati, Serikali haitomvumilia kwani atakuwa anaharibu taswira nzuri ya ofisi yake ikiwa ni pamoja na taswira ya Mhe. Rais ambaye amehimiza Watumishi katika Taasisi zote za kupata stahili zao.

Kwa niaba ya Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mhe. Seleman Mzee amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuwahimiza kutekeleza majukumu yao kikamilifu hususani suala la uzingatiaji wa masilahi ya Watumishi wa Umma mkoani Mtwara.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa ufafanuzi wa hoja za kiutumishi zilizowasiliswa na baadhi ya Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi na Viongozi walio katika mkoa huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Bi. Changwa Mkwazu akiwasilisha hoja za kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na Viongozi hao waliopo mkoani Mtwara.

Mhe. Mzee ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo waliyowapewa na Mhe. Ndejembi mara watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi na kuongeza kuwa, watatoa kipaumbele kwenye suala la masilahi ya Watumishi wa Umma ili kuwajengea watumishi ari ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa lengo la kutoa huduma bora kwa umma.

Mhe. Ndejembi, amefanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi waliopo katika Taasisi za Umma mkoani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news