Wanaosimamia zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini watakiwa kutenda haki

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini kutenda haki na kutokuwa na upendeleo wa aina yoyote wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo linaloendelea katika Halmashauri mbalimbali nchini,anaripoti James K. Mwanamyoto-Mtwara.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Bw. Hamisi Mkonga (wa kwanza kushoto) mkazi wa Mtaa wa Haikata, Manispaa ya Mtwara Mikindani aliyefanyiwa utambuzi ili kuandikishwa katika orodha ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Mhe. Ndejembi amesema hayo kwa wawezeshaji wa zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuangalia namna zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini linavyoendeshwa katika manispaa hiyo.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Mwenyekiti wa Mtaa, Mtendaji wa Mtaa na Mtendaji wa Kata ni viongozi muhimu wanaotegemewa na Serikali kusimamia kikamilifu zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini, ili kuondoa uwezekano wa kuwepo malalamiko ya upendeleo au kutotendewa haki kaya maskini ambazo ndio walengwa wakuu wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wa pili kutoka kushoto) akielekea katika moja ya kaya maskini iliyopo Mtaa wa Haikata, Manispaa ya Mtwara Mikindani inayofanyiwa utambuzi ili kuandikishwa katika orodha ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisalimiana na baadhi ya Watendaji wa Manispaa ya Mtwara Mikindani waliopewa jukumu la kufanya zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini zitakazonufaika na Mpango wa TASAF katika Manispaa hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa zoezi hilo.

“Dirisha la utambuzi na uandikishaji likifungwa na zikaachwa kaya zinazostahili kupata ruzuku, kaya hizo zitaibua malalamiko na kuwasilisha malalamiko hayo Serikalini kupitia kwa Wakuu wa Wilaya au Wakurugenzi Watendaji jambo ambalo litatia doa azma ya Serikali ya kuziwezesha kaya maskini kuboresha maisha yao”, amehimiza Mhe. Ndejembi.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka waliopewa dhamana ya utambuzi na uandikishaji kaya maskini kuwa waadilifu kwa kuweka kando tofauti walizonazo na walengwa wa mpango wa TASAF ili kutenda haki, na kuongeza kuwa, hategemei kusikia kuna kaya yoyote maskini ambayo haijaandikishwa kutokana na sababu ya kutokuwa na uhusiano mzuri baina ya watendaji wa Serikali na walengwa.
Baadhi ya watendaji wa Manispaa ya Mtwara Mikindani waliopewa jukumu la kufanya zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini zitakazonufaika na Mpango wa TASAF katika Manispaa hiyo, wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa zoezi hilo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani COL. Emmanuel Mwaigobeko akiwasilisha taarifa ya zoezi la utambuzi na uandikishaji wa Kaya Maskini kwa Mhe. Ndejembi, ambazo zitanufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa hiyo.
Meneja wa Uhawilishaji Fedha wa TASAF, Bw. Selemani Masala amemshukuru Mhe. Ndejembi (hayupo pichani) kwa kufanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na watendaji wanaosimamia zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Serikali kupitia Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 iliahidi kuboresha maisha ya kaya maskini nchini, hivyo kaya zote zenye sifa ya kupata ruzuku zitendewe haki kwa kuandikishwa, kinyume na hilo wasimamizi wa zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini watakuwa wanakwenda kinyume na azma ya Serikali.

Kwa upande wake, Meneja wa Uhawilishaji Fedha wa TASAF Bw. Selemani Masala amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na watendaji wanaosimamia zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Bw. Masala amesema, kitendo cha Mhe. Ndejembi kuwahimiza watendaji kutenda haki katika utambuzi na uandikishaji wa kaya kinawakumbusha watendaji hao kuwa waadilifu katika kutekeleza zoezi hilo.

Zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani linafanyika katika mitaa 75 ambayo haikuwepo kwenye Mapango wa Kunusuru Kaya Maskini kipindi cha kwanza. Ili kuhakikisha mitaa yote 75 inafikiwa, utambuzi umepangwa kufanyika kwa awamu nne kuanzia Aprili 25, 2021 na kukamilika Mei 6, 2021.

Post a Comment

0 Comments