HOPE FOR GIRLS AND WOMEN TANZANIA WAWAPIGA MSASA WAKULIMA, WAWAPA SIMU JANJA MKOANI MARA

Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalojihusisha na utoaji wa hifadhi kwa wasichana ambao hukimbia ukatili wa kijinsia Mkoa wa Mara limeendesha mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa wakulima 60 wa Wilaya ya Butiama na Serengeti pamoja na kuwapa simu janja 60 zenye thamani ya Shilingi Milioni 30 zitakazowasaidia kutambua magonjwa yanayokabili mazao mbalimbali yakiwemo mihogo na mahindi, ANARIPOTI AMOS LUFUNGULO (DIRAMAKINI) Mara.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly (aliyenyoosha mkoano) akiwa na baadhi ya wakulima wa Kata ya Kukirango Wilaya ya Butiama wakitumia simu janja katika mafunzo ya vitendo kubaini iwapo kuna ugonjwa katika mazao zao la muhogo.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa nyakati tofauti ambapo katika Wilaya ya Serengeti yametolewa kwa wakulima wa Kata ya Matare na Wilaya ya Butiama yametolewa kwa Wakulima wa Kata ya Kukirango, yanalengo la kuwasaidia Wakulima hao, kuweza kuendesha shughuli zao za kilimo kwa ufanisi pamoja na kutoa elimu hiyo kwa Wakulima wengine katika maeneo yao jambo ambalo litachagiza uzalishaji wa mazao kwa tija.

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly ambaye amewahi kutunukiwa Tuzo ya heshima ya Malkia wa Nguvu kutokana na juhudi zake za kutetea haki za Binadamu na Kupambana na Ukatili wa Kijinsia akizungumza wakati wa utoaji simu hizo April 30, 2021 amesema, wameamua kutoa elimu hiyo na simu hizo zilizounganishwa na teknolojia ya kisasa ili kupata maarifa yatakayowasaidia kutambua Magonjwa ya mazao mbalimbali na namna ya kukabiliana nayo, na zitatumika kwa kazi hiyo pekee kwa tija ya kuwaongezea kipato.

Pia, Rhobi amewaasa wakulima hao kuwasehemu muhimu ya kushiriki kuunga mkono mapambano ya Ukatili wa Kijinsia kwa kuhimiza usawa hasa katika umiliki wa rasilimali baina ya mwanamke na mwanaume ngazi ya familia ikiwemo kufanya maamuzi ya pamoja katika matumizi ya mazao yanayozalishwa kwa manufaa ya wote.
"Mkulima kama amesahau ugonjwa akienda na simu yake shambani akaiweka kwenye mmea atatambua ugonjwa huo na kuchukua hatua ya kuwaona wataalamu. Na pia kila mkulima aliyepata elimu hii na simu atakwenda kuunda Kikundi cha wakulima wenzake kuanzia 10 ili kuwapa elimu. Mkulima akiwa na mazao mazuri hata Ukatili wa Kijinsia unapungua katika familia shabaha yetu kubwa ni kuona Ukatili unaisha Kutoka na uzalishaji wenye tija."

Naye Salome Joseph Afisa Kilimo wa Kata ya Kukirango amesema kuwa, simu hizo zitasaidia kuongeza uzalishaji mazao kwa tija kwani wakulima watapata taarifa mbalimbali muhimu zitakazowasaidia kufanya kilimo cha tija na kuondokana na kilimo cha mazoea ambacho wamekuwa wakikifanya kutokana na uchache wa Maafisa Kilimo ndani ya kata hiyo.

Prisila Samwelly Mgendi Mkulima Kutoka kata ya Kukirango amepongeza Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kupitia Mkurugenzi wake Rhobi Samwelly, kwani mbali na simu hizo kuwasaidia kupata maarifa kuhusiana na kilimo Bora, zitasaidia pia kutoa taarifa za Ukatili wa Kijinsia na hivyo wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi na haki za binadamu.

Mazara Kizibo Mazara ambaye ni Mkulima wa mazao mchanganyiko katika kata ya Kiabakari, amesema kutokana na uchache wa Maafisa Kilimo katika kata hiyo atakuwa sehemu muhimu ya kuwaelimisha wengine ambao hawajui Magonjwa mbalimbali na mbinu bora za kilimo walizofundishwa katika mafunzo hayo.

Katika semina hiyo, wakulima hao wamefundishwa namna ya kuandaa shamba, magonjwa mbalimbali yanayokabili mazao hususan mihogo na mahindi, hatua ya upandaji, utunzaji mazao hadi hatua ya mavuno. Huku wakiombwa kuzingatia kilimo chenye tija kwa kulima walau eneo dogo lakini mavuno yawe mengi na yenye ubora unaotakiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news