Khatib Said Haji awaliza Wabunge

KUFUATIA kifo cha aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Konde kisiwani Pemba,Khatib Said Haji wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamehuzunishwa na kifo hicho huku wakitoa maoni yao jinsi alivyokuwa akichangia hoja za maendeleo ya nchi licha ya kwamba alikuwa chama cha ACT Wazelendo,anaripoti Doreen Aloyce,Dodoma
Kifo cha mbunge huyo kilitokea jana Alfajiri katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar Es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ambapo hivi karibunu hakuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na kuumwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wabunge hao katika viwanja vya Bunge mara baada ya kuahirishwa vikao vya Bunge jana ambavyo vilikuwa vinaendelea jijini hapa walisema kifo cha mwenzao kimekuwa cha kushtukiza kwani ni mapema tangu achaguliwe na wananchi wake.

Mbunge Stella Manyaya Jimbo la Nyasa alisema kuwa alikuwa nae kwenye kamati ya viwanda na biashara ambapo alichangia michango mizito iliyolenga katika kutahadharisha,kushauri mabadiliko katika kujenga nchi ya Tanzania katika uchumi.

Kwa upande wake Mbunge wa Geita mjini Costantine Kanyasu alisema kuwa kifo hicho kimekuwa cha mahuzuniko makubwa kwani alikuwa mtu wa watu, alikuwa mcheshi mwenye utani mwingi hali ambayo ilimfanya kuwa na marafiki wengi kwa muda mchache waliokutana nae Bungeni.

‘’Namfahamu vyema ni mbunge ambaye alikuwa na mahusiano mazuri nje ya bunge alikuwa mcheshi utani na ndani ya bunge alikuwa ni mtetezi mzuri wa chama chake hata wakati wa mgogoro wa Lipumba walisimama imara kumkataa Lipumba kwa kusaliti chama chake alikuwa mtu wa msimamo.’’alisema Kanyasu.

Mbunge Masache Kasaka Jimbo la Lupa Chunya (CCM) alisema ‘’Nimesikitika sana na kifo hiki imekuwa ni kilio kwa wabunge wote ni mbunge ambaye alikuwa hajafungamana na chama chochote, alikuwa ni kiongozi kwenye jamii kwani alikuwa haiegemei upande wowote huku akitoa hoja za mashiko kwa maslahi ya nchi yetu,"amesema.

Stephen Kiluswa mbunge jimbo la Longido alisema kuwa, alipopata taarifa za kifo hicho kilimshtua kwani hakujua kama ana matatizo ya kiafya huku akidai kuwa alikuwa mpinzani ambaye alichangia hoja zenye tija kwa jamii tofauti na wapinzani wengine ambao hata jambo zuri wao wanapinga lakini yeye alipinga kwa tija na maslahi ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news