KMC FC KUONDOKA NA WACHEZAJI 22 KESHO KUWAFUATA NAMUNGO RUANGWA

Kikosi cha wachezaji 22 wa KMC FC kitaondoka jijini Dar es Salaam kesho asubuhi kuelekea Ruangwa mkoani Lindi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Namungo utakaochezwa siku ya Jumapili ya Mei 9 katika Uwanja wa Majaliwa Mkoani humo.
Kikosi hicho cha wana Kino Boys , kinakwenda kukutana na Namungo kwa mara ya pili katika msimu huu wa 2020/2021 huku KMC FC ikiwa ugenini ambapo awali katika mchezo ambao walikutana katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam ikiwa mwenyeji kikosi hicho kilipata ushindi wa magoli matatu kwa sifuri.

Hadi sasa Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, imeendelea kujifua kuelekea katika mchezo huo ambapo pamoja na mambo mengine inajipanga kuhakikisha kwamba inakwenda kufanya vema na hivyo kupata alama tatu muhimu.

KMC FC chini ya Kocha Mkuu John Simkoko pamoja na msaidizi wake Habibu Kondo wameendelea kukisuka kikosi hicho sambamba na kurekebisha makosa mbalimbali ambayo yalijitokeza katika mchezo wa michuano ya kombe la Shirikisho la Azam na hivyo kupelekea kutolewa katika michuano hiyo dhidi ya Dodoma Jiji ikiwa ni katika hatua ya kuweka mikakati kwa timu ili iweze kufanya vizuri katika mchezo huo.

“Tunakwenda ugenini kukutana na Ttimu ambayo kimsingi inajua kuutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani, lakini pia tumeona wametoka kupoteza mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania, hivyo mchezo utakuwa mgumu lakini kikubwa tunakwenda kupambana ili kuhakikisha kwamba kama Timu tunaondoka na matokeo mazuri,"amesema.

Hata hivyo, katika mechi za Ligi Kuu soka Tanzania bara ambazo KMC FC imewahi kukutana dhidi ya Namungo, ikiwa ugenini KMC FC ilipoteza mchezo wake mmoja kwa kufungwa magoli mawili kwa moja ,huku Namungo wakipoteza michezo miwili wakiwa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Imetolewa leo Mei 6
Na Christina Mwagala

Afisa Habari na Mawasiliano wa Timu ya KMC FC

Post a Comment

0 Comments